Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
DIWANI wa Kata ya Kitunda, Victor Vedasto amesema barabara korofi katika kata yake zimekuwa kero kila kipindi cha mvua hali inayosababisha gharama za usafiri pia kupanda.
Amesema hayo leo asubuhi wakati akikagua barabara zilizowekwa mawe kwa ajili ya kuwezesha wananchi na magari kupita kwa urahisi .
“Barabara ni changamoto, nipo barabarani kuhakikisha mawe yanawekwa vizuri kufukia mashimo, natamani sana barabara zirekebishwe kwa kiwango ambacho hazitaharibika katika vipindi vya mvua.
“Sasa hivi barabara nne tayari zimeshapata mkandarasi wa kufanya marekebisho katika maeneo korofi, wataweka zege katika baadhi ya maeneo ya barabara hizo,”amesema.
Alizitaja barabara zinazitarajiwa kufanyiwa marekebisho kuwa ni Kitunda-Machimbo, Masai-Mpalange, Masai-Kipera na Kitunda-Mzinga.
Amesema changamoto nyingine wanayokabiliana nayo Kata ya Kitunda ni stendi kwa ajili ya daladala, bajaji na pikipiki na eneo kwa ajili ya soko.
“Changamoto zingine zimeshulikiwa ikiwemo kupata eneo la kujenga shule ya Sekondari, eneo limepatikana Relini na mwenye eneo alishalipwa jumla ya Sh 387,000,000.
“Sh milioni 500 tayari zimetolewa kwa ajili ya ujenzi, Sh milioni 17 zimetumika kupima udongo katika eneo hilo na ilitarajiwa ujenzi uanze mwezi huu Desemba,”amesema Victor.