Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
Msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo, ‘Ommy Dimpoz’, amefunguka jinsi Alikiba alivyomsaidia kwenye maisha yake ikiwamo kumuuguza.
Akizungumza wakati wa Listening Party ya Albam ya Mfalme wa Bongo Fleva, AliKiba ya ‘Only one King’ usiku wa kuamkia leo katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Ommy Dimpoz amefunguka kuwa mbali na kushirikiana kwenye wimbo ya NAINAI kuna mambo mengine mengi ambauyo watu hawayajui.
“Ukiacha na historia yetu ya wimbo wa Nai nai iliyonitoa kwenye gemu, wakati napitia matatizo ya kiafya tulikuwa hapa Serena kwenye kamati ya harusi yake tukatoka tukaenda kula sehemu baada ya kula chakula kilinikwama.
“Kilivyonikwama tulikuwa na Alikiba na Gavana Ali Hassan Joho wa Mombasa, Ali aliingiwa na huzuni alipoona napata shida kula akasema tutafanyaje akamwambia Gavana najua unamadokta wazuri sana Kenya nanaona ndugu yangu anateseka kweli hata hii harusi yenyewe hana hata raha nayo,”amesema Ommy Dimpoz.
Staa huyo wa Tupogo ameendelea kusema kuwa: “Gavana akampigia Daktari, akasema niende anione ndo safari yangu ya matibabu ilipoanzia pale nilipoenda kule nikakutana na upasuaji, upasuaji, upasuaji mpaka leo hii stori za amekufa amefariki lakini watu walijuwa hawaelewi sababu ya mimi kupona ntawaambia kitu kimoja.
“Kupona kwangu na Mungu kunipa maisha mapya Ali yupo nyuma yake hivyo mimi Ali hata itokee nimemfumania na mke wangu nimeshamsamehe,” amesema Ommy Dimpoz huku akidai anatania huku mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinjuma ”Mwana FA’ akitania kuwa aache uchawa.