Na JUSTIN DAMIAN, NORTH CAROLINA MAREKANI
JERRY William (35), Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyekuwa mkazi wa hapa Asheville North Carolina, aliuawa na polisi mweupe (mzungu) Julai mwaka huu kwa kupigwa risasi mara nne baada ya kufukuzwa na polisi na kuingia kwenye sehemu yenye majengo mengi.
Alipokuwa akijaribu kutoka na gari lake, alipigwa risasi mara nne na ofisa wa polisi aliyedai kuwa marehemu huyo alitoa bunduki akidhamiria kumshambulia.
Hata hivyo, mashuhuda kadhaa wa tukio hilo walisema marehemu hakuwa na silaha na hakuna shahidi yeyote aliyejitokeza kusema kama ni kweli alikuwa na bunduki. Mwili wa kijana huyo ulionekana na mashahidi ukiwa umelala pembeni ya kokoto ukiwa na damu nyingi huku bunduki ikiwa pembeni yake.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema polisi waliiweka kwa makusudi bunduki hiyo kuonyesha kuwa alikuwa na silaha.
Baadaye polisi wenye silaha walifika katika eneo la tukio ambapo walikaa kwa saa kadhaa huku wakimzuia mama mzazi wa Jerry, Najiyyah Avery, kuona mwili wa mwanawe.
Mama huyo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema mauaji ya kijana wake huyo yalikuwa ni uonevu wa polisi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. “Kijana wangu hakuwa mtu wa vurugu hata siku moja, alikuwa ni Mmarekani aliyefanya kazi kwa bidii na kuitunza familia yake,” alisema mama huyo aliyekuwa akitokwa na machozi.
Kutokana na tukio hilo, kulikuwapo na maandamano yaliyofanyika kupinga tukio hilo na mengine ya aina hiyo. Ibada ya kumwombea marehemu pia ilifanyika huku viongozi wa dini wakipaza sauti zao kumwomba Mungu aepushe roho ya kibaguzi na mauaji kama hayo.
Mwandishi wa makala haya aliyepo katika mji huo alipata bahati ya kushiriki moja ya maandamano ya amani ya kupinga ubaguzi na mauaji yaliyofanyika katika mji wa Asheville.
Maandamano hayo yaliandaliwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali yakiwa na ujumbe “maisha ya watu weusi yana thamani,”.
Mchungaji wa Kanisa la Nazareth First Missionary alimwambia mwandishi wa makala hii kuwa, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kuona Marekani ikifumbia macho suala la mauaji ya watu weusi yanayofanywa na polisi weupe.
Alisema Mungu amewaumba binadamu wote sawa kwa mfano wake na kama kanisa wanasikitishwa kuona polisi wakiwaua binadamu wenzao, huku serikali ikishindwa kuchukua hatua kali kukomesha vitendo hivyo.
Akisoma tamko hilo mbele ya Makao Makuu ya Idara ya Polisi, mchungaji huyo alisema ripoti iliyotolewa na Polisi kuhusu mauaji ya Jerry Williams haitaweza kuponya majeraha yaliyo katika mioyo ya wapenda haki.
“Tukiwa kama viongozi wa dini tunakemea vitendo vya mauaji kwa watu weusi na ubaguzi unaojitokeza kwenye elimu, kazi, kupata haki za kisheria na jamii kwa ujumla. Tunataka wale walio kwenye ngazi za juu za haki kama polisi na mahakama wachukue hatua za haraka,” anasema.
Theo Noel ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika ambaye ni mmoja kati ya wahanga wa sera za kibaguzi katika taasisi mbalimbali za umma hapa Marekani.
Theo, ambaye anaendesha maisha yake kwa kutengeneza pizza, anasema alifukuzwa shule akiwa High School kwa kosa ambalo halikustahili kufukuzwa na kuanzia hapo ilibidi atafute kazi kwa ajili ya kuweza kujikimu kimaisha.
“Shule niliyokuwa nikisoma tulikuwa weusi wachache sana, walimu hawakutupenda hata kidogo kwa sababu tu ya rangi yetu. Mimi pamoja na wenzangu wawili tulifukuzwa kwa sababu ambayo haikustahili kufukuzwa,” anaeleza.
Kijana huyo alionyesha kusikitika kwa namna ambavyo amekuwa akibaguliwa na kutamani kuwa angekuwa Afrika ambako ni chimbuko lake na kuishi maisha yasiyo na ubaguzi.
“Kazi yangu ni kutengeneza pizza, kazi ambayo ni ya mwisho kabisa, hawakuniruhusu nisome hata niwe mwalimu wa chekechea, hii ndiyo Amerika,” alisema kwa uchungu.
Theo, ambaye alikuwa ametoka kupiga kura wakati akiongea na mwandishi wa makala haya, alisema hakuwa amemchagua rais kwa kuwa hakuona ambaye angemfaa.
“Wamarekani weusi wengi tulimpigia kura Rais Obama tukiamini angeweza kutufanya tutambulike kama raia wa Marekani na kupata stahiki zote anazotakiwa kupata raia wa Marekani. Obama hajaongea wala kufanya chochote juu ya sisi weusi ambao ni zaidi ya watumwa katika nchi yetu.
“Kama Obama ambaye pia amepitia baadhi ya adha ambazo tunapitia ameshindwa kubadilisha hali, ni wazi kuwa sisi weusi tutaendelea kuishi maisha duni yasiyo na tumaini. Ni muda muafaka kwa sisi kuanza kutafuta asili yetu ilipo Afika na kwenda kuishi huko kwa sababu hapa Marekani tunauawa, tunabaguliwa, tunafanyiwa kila baya na polisi.”
Kwa kipindi cha mwaka 2015 Wamarekani weusi wasio na silaha zaidi ya 102 wameuawa na polisi weupe, ikiwa ni takribani watu wawili kila siku. Mmoja kati ya watu watatu weusi waliouawa na polisi hapa Marekani kwa mwaka 2015 hawakuwa na silaha na namba hii inaweza kuwa kubwa kutokana na matukio mengi kutoripotiwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 37 ya watu wasiokuwa na silaha waliouawa na polisi mwaka 2015 walikuwa ni Wamarekani wenye asili ya Afrika, japokuwa wanachukua asilimia 13 ya idadi ya watu hapa Marekani.
Jambo jingine la kushangaza ni kuwa, kati ya kesi za mauaji ya watu 102, ni kesi kumi tu ndizo zilifunguliwa za mauaji na wahusika kupelekwa mahakamani na ni kesi mbili tu ndizo zilizotolewa hukumu.
Katika kesi ya kwanza iliyohusisha mauaji ya Mathew Ajibade, alifungwa kifungo cha mwaka mmoja jela na Mahakama ilimruhusu kuwa anatumikia kifungo chake siku za mwisho wa wiki, yaani Jumamosi na Jumapili. Ofisa mwingine wa Polisi aliyehusika na kifo cha Eric Harris bado hajahukumiwa.