26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

DENI LA TAIFA LAWATISHA WABUNGE

Na MAREGESI PAUL, DODOMA

KASI ya ukuaji wa deni la Taifa, ambalo hadi Juni 2016 lilifikia Dola za Marekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na Dola bilioni 19.69 Juni 2015 limewatisha wabunge.

Hilo lilionekana jana wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha kuanzia Januari 2016 hadi Januari 2017.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Josephat Kandege, ilisema pamoja na Serikali kusema deni hilo ni himilivu, bado linatumia fedha nyingi za makusanyo ya kila mwezi.

Aliyekuwa wa kwanza kuonesha hofu hiyo ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ambaye alisema kuna haja deni hilo kufanyiwa tathmini upya ingawa Serikali inasema bado linahimiliwa.

“Deni la Taifa tunaona jinsi linavyokua. Kwa hiyo, naomba Serikali ilitathmini kwa kupitia mapato yetu ya ndani kwa sababu tutalilipa kupitia kodi tunazowatoza Watanzania. Pamoja na hayo, umefika wakati sasa Serikali ichukue hatua kuokoa bajeti yetu kwa sababu hatuwezi kuwa na bajeti inayotegemea fedha za wafadhili,” alisema Bashe.

Wakati Bashe akisema hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), alisema kama Serikali haitachukua hatua ya kukabiliana na deni hilo, litaweza kukwamisha shughuli za Serikali.

“Deni la Taifa lisipoangaliwa upya, linaweza kukwamisha shughuli za Serikali ingawa tunaambiwa bado linahimilika kwa vigezo vya Benki ya Dunia na IMF. Deni hilo lazima liangaliwe kwa kutumia mapato ya ndani, kwa sababu hata sasa tukimuuliza Waziri wa Fedha kwamba mwezi ujao atalipa kiasi gani, hawezi kujua,” alisema Serukamba.

Pamoja na hayo, mbunge huyo alionesha kutoridhishwa na tabia ya Serikali kueleza jinsi biashara mbalimbali zinavyofungwa nchini.

Kwa mujibu wa Serukamba, biashara zinavyofungwa ni dalili ya Serikali kukosa mapato, hivyo akataka wafanyabiashara wanaokwepa kodi, wasifungiwe biashara bali waitwe na kuelezwa jinsi wanavyotakiwa kulipa kodi wanazodaiwa. 

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini, Athony Komu (Chadema), alisema kasi ya ukuaji wa deni la Taifa inatisha na kwamba lazima wabunge wachukue hatua kabla Serikali haijafikia hatua ya kutokopesheka.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Phillip Mpango, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja hizo, kuwa deni ta Taifa linakua kwa sababu ni la muda mrefu.

“Hapa wapo waliosema deni la Taifa linakua na wanasema tunajikita zaidi kulipa mikopo ya nje. Kimsingi, Serikali haielezi kulipa madeni ya nje tu na kuwaacha wadeni wa ndani. Pia, ieleweke kwamba deni la Taifa ni la muda mrefu na kuna madeni mengine ni ya tangu enzi za uhuru. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kulilipa kadiri inavyoweza,” alisema Dk. Mpango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles