Mwandishi wetu, Arusha
Shirika la Kimataifa la watetezi wa haki za Binaadamu la Defend Defenders na Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC), wamewataka wanahabari kufanya kazi kwa weledi huku wakijali afya zao.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku Tano ya wanahabari jijini Arusha, Kuhusiana afya ,kuondoa msongo wa mawazo na uandishi Bora wa habari za Uviko-19, Afisa Kitengo ya Ulinzi na Ustawi wa shirika laDefendDefenders East and Horn of Africa, Karis Moses alisema wanahabari ni kazi nzuri na inachangamoto nyingi.
Moses alisema kazi za uandishi wa habari na utangazaji zinakawaida kuwa changamoto ambazo husababisha msongo wa mawazo na bila kupata tiba usababisha Maradhi hivyo ni muhimu sana kujali afya zao.
“Kazi zenu ni ngumu na mnapaswa kuwa na utaratibu za kukabiliana na changamoto za kisaikolojia ambazo kama hazifanyiwi kazi huwezi kusababisha Maradhi ambayo yataathiri utendaji kazi wetu “alisema
Muuguzi Sam Sangalo alisema ni muhimu wanahabari kutenga muda wa kupumzika ,kufanya mazoezi,kupata lishe bora na kujiepusha na mambo ambayo yatawapa msongo wa mawazo wenye athari kwao.
Mjumbe wa bodi ya shirika la watetezi wa haki za Binaadamu Tanzania(THRDC) Edwin Soko akifungua mafunzo hayo aliwataka wanahabari kufanya kazi Kwa weledi ili kazi Yao iwe na tija katika jamii.
Soko alisema jamii kwa kawaida ina imani kubwa na wanahabari wanaojitambua kama ndio watetezi wao kutokana na kupaza sauti zao na kuibua changamoto zao ili serikali na Wadau wengine wazifanyie kazi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC),Mussa Juma alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha wanahabari wajibu wao katika jamii lakini pia kujali afya zao.
Juma alisema wanahabari wakijua wajibu wao katika jamii watasaidia kupunguza changamoto ikiwepo upotoshwaji juu ya ugonjwa wa uviko-19 na Chanjo na hivyo Wananchi wengi kujitokeza kupata chanjo.
Waandishi wa habari 20 Kutoka mikoa Saba wanashiriki mafunzo hayo ambayo yatakwenda sambamba na kupata chanjo ya Uviko-19 , kutembelea hifadhi ya Taifa kujifunza na kujifunza uchoraji kama njia pia kupunguza msongo wa mawazo.