*Watuhumiwa 72 wadakwa
Na Esther Mnyika Mtanzania Digital
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ikiwemo Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imekamata kilo 54,506.553 za dawa za kulevya wakiwemo watuhumiwa 72.
Akizungumza leo Aprili 4,2024 jijini Dar es Salaam na Waandishi wa Habari, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa na dawa hizo ni kupitia oparesheni iliyofanyika katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.
Amesema dawa hizo zinajumuisha mashamba na viwanda pamoja na kuteketeza ekari 262 za mashamba ya bangi.
“Dawa zilizokamatwa ni bagi kilo 54,489.65, mirungi kilogramu 10.3, heroin na cocaine gramu 1.98.
“Nyingine ni kilogramu 4.623 aina mpya ya dawa ya kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDP) iliyokamatwa jijini Dar es Salaam ikisafirishwa na raia wa Comoro anaitwa, Ahmed Bakar Abdou (32),” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Amesema watuhumiwa 72 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema methylene dioxy pyrovalerone(MDP) ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu.
Amesema dawa hiyo ina kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji ilikilinganishwa na dawa nyingine za kulevy na imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, haroin na methamphetamine.
Ameeleza kuwa dawa hiyo ya kulevya huuzwa kwa njia ya mtandao na husafirishwa kipitia kampuni za usafirishaji vifurushi hufichwa kwa kuweka chapa za majina bandia kama vile bath salts, ivory wave, plant fertilizer, vanilla sky na energy.
Pia amesema mamlaka hiyo imebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga na Mabatini mkoani Tabora ambapo wahalifu hao wamekata miti katikati ya misitu hiyo na kulima bangi.
Amesema kwa ushirikiano waliopata kutoka kwa TFS walifanikiwa kuteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusiki.
“Tunatoa shukurani zetu kwa wananchi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu wazalishaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao na tutaendelea kushirikiana na wadau na jamii kwa ujumla ili kufanikisha oparesheni zetu,” ameongeza.