24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

DC Nyamagana awatoa hofu wananchi usalama wa chanjo ya corona

Na Clara Matimo, Mwanza

Kufuatia uwepo wa maneno mengi yanayoleta hofu kwa wananchi juu ya uchanjaji wa chanjo ya corona inayotarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni nchini kwa makundi maalulum, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, amewatoa wasiwasi wananchi juu ya usalama wa huduma hiyo na kuwataka kuiamini Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina  Makilagi, akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) nje ya ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya kuhudhuria kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe, chanjo ya corona, huduma za kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na huduma ya afya ya mama na mtoto kilichoandaliwa na uongozi wa Mkoa huo. Picha na Clara Matimo.

Amina ametoa kauli hiyo leo, Julai 27 jijini hapa alipozungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuhudhuria kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe, chanjo mpya ya corona, huduma za kudhibiti maambukizi ya virusi vya  ukimwi pamoja na huduma ya afya ya mama na mtoto kilichoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Mwanza.

Amesema serikali haiwezi kufanya jambo baya kwa wananchi wake wala kuwapa chanjo ambayo itawaletea madahara kwani wajibu wake ni kuwalinda raia wake.

 “Watanzania wenzangu nawaomba wapuuze maneno ya baadhi ya watu wanayoyatoa kuhusu athari za chanjo hiyo kwanza watambue kwamba chanjo zote tunazochanjwa Tanzania ziwe za watoto au za mama wajawazito zinatoka nje ya nchi hakuna chanjo inayotengenezwa hapa nchini   kwa hiyo mimi nawaambia wananchi wasiwe na wasiwasi wawapuuze hao wanaowatisha.

“Mataifa yaliyotengeneza  chanjo ya Covid-19 yamekuwa yakishirikiana  na nchi yetu  muda mrefu katika chanjo mbalimbali pamoja na kutugawia  bure vidonge vya ARV ambavyo vinawasaidia waliopata maambukizi ya virusi vya ukimwi wangekuwa na dhamira mbaya ya kutuuwa wengi tungeishakufa maana chanjo zao nyingi tumeishachanjwa,  mimi ninaongea nikiwa na ushahidi maana nimehudumu katika kamati ya masuala ya ukimwi,”amesema na kuongeza:

“Mimi binafsi nitakuwa  mtu wa kwanza  kuchanjwa katika Wilaya ya Nyamagana kwa kuwa  nimeelezwa faida zake nimeridhika na ninajua Rais wetu Samia Suluhu Hassan,  anania ya kutulinda  wananchi wake ili tusipate maambukizi ya  ugonjwa wa corona ndiyo maana ametuletea chanjo hii tena kwa hiari sio lazima hivyo ni wajibu wetu kuiamini Serikali yetu na viongozi wake,”amesisitiza.

 Amewataka wananchi kutambua kwamba watakapochanjwa watakuwa wamejikinga pia hawatapata maambukizi ya ugonjwa huo  kwa sababu watakuwa na kinga ambayo itawasaidia kuwaweka salama zaidi.

“Naamini  baada ya sisi  wananchi wa awamu ya kwanza kupata chanjo, kadri tutakavyoendelea watanzania wenzetu wakiona matokeo ambayo kwa hakika yatakuwa ni mazuri nao watakuja kuchanjwa bila wasiwasi  kwa sababu  watakuwa wameishaona mafanikio kwa sisi tuliotangulia,”amesema.  

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema maandalizi ya kutoa chanjo hiyo ya corona yanaendelea vizuri na wameisha ainisha  vituo vya kupambana na corona kwa njia ya chanjo huku naye akiahidi kuwa wa kwanza kuzindua chanjo hiyo mkoani humo kwa kuchanjwa.

“Mimi natambua faida za chanjo hiyo, hivyo nitakuwa wa kwanza kuchanjwa nawaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza wajitokeze kwa wingi baada ya uzinduzi ili nao wachanjwe waweze kujikinga na maambukizi wasiwasikilize watu wasio na utaalamu wa masuala ya afya.

“Sasa hivi kila mtu ni mtaalamu wa masuala ya afya kumekuwa na siasa nyingi mno chafu  kila mtu anazungumza kama ni mtaalamu wa masuala ya afya sielewi lengo lao ni nini hao ndiyo wenye nia ya kuwapotosha watanzania ili waangamie lakini viongozi wa Serikali tutaendelea kuwapa elimu  watambue kwamba chanjo ni salama kabisa na nia ya serikali ni kuwalinda,”amesema Mhandisi Gabriel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles