Renatha Kipaka, Muleba
Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila, amezindua rasmi soko la Dagaa la Magarini lililopo kijiji cha Katembe litakalochochea mapato ya ndani ya halmashauri kwa asilimia 51.
Akizindua soko hilo juzi, Nguvila amesema soko hilo limeruhusiwa kufanya biashara ndani na nje ya nchi na kuwaeleza wananchi kuwa wilaya imepokea barua kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Desemba 20, 2021 ikiruhusu biashara ya dagaa kusafirisha ndani na nje.
“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa soko letu la Magarini limekuwa la kimataifa, wafanyabiashara wote mnakaribishwa, mnaotaka kuweka maduka ya jumla njooni mjenge ili watu wa visiwani wasipate tabu ya kwenda mbali kununua bidhaa, mjenge hoteli na hata maduka ya jumla ya vinywaji ili magarini ichangamke,” amesema Nguvila.
Aidha, Nguvila amewahimiza viongozi wa eneo hilo kuwakaribisha wafanyabiashara mbalimbali ambao watataka kuja kufanya biashara huku akimhimiza Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani wote pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha wanasimamia vyema mapato hayo ya halmashauri ili yaweze kuonekana kwani kulikuwa na upotevu wa mapato ambayo yalikuwa yanakwenda wilaya zingine.
“Nendeni mkaweke utaratibu mzuri wa namna ya kusimamia mapato ya Halmashauri ili heshima ya wilaya ya Muleba iendelee kuwa juu na ninyi wafanyabiashara tusiingie katika mkumbo wa kukwepesha mapato. Tukikosa kukusanya mapato tutakuwa wa ajabu sana, kwa hiyo natamani kuona mapato yanapanda,” amesema Nguvila.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila, ameeleza kuwa tangu Septemba, mwaka huu zilipowekwa nguvu za kuanzishwa kwa soko hilo tani 760 zimeweza kupita katika soko hilo ambapo zaidi ya tani 510 zimeweza kutoka katika kata mbili tu ambazo ni Mazinga na Ikuza na tani 250 zimetoka nje ya wilaya ya Muleba na kupita katika soko la Magarini.
Amesema kuwa miongoni mwa tani hizo 760 tani 630 zimesafirishwa na kupelekwa katika nchi ya Uganda na Rwanda na nyingine kusafirishwa ndani ya nchi kwenda mikoa mbalimbali. Hivyo, halmashauri inakwenda kupata ushuru wa uhakika.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Magongo Justus amewasihi wananchi kuendelea kulitumia eneo hilo kwa manufaa yao na kwa manufaa ya Halmashauri ambapo ameongeza kwa kuwaomba wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano wa kutosha pale serikali itakapoanza kuboresha zaidi ya hapo.