MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Filbert Sanga amesema ukaguzi pamoja na elimu inayotolewa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) vimechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali katika sehemu za kazi katika wilaya yake.
Sanga ameyabanisha hayo leo alipofanya ziara katika ofisi za OSHA za jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi taasisi hiyo ya umma inavyotekeleza majukumu yake ambayo yanalenga kulinda afya ya mfanyakazi pamoja na mali za wawekezaji ili kuleta tija katika uzalishaji.
“Nianze kupongeza kazi kubwa mnazozifanya ambazo zimeleta mabadiliko makubwa sana katika sehemu nyingi za kazi. Huko nyuma kabla ya uwepo na maboresho kwenye taasisi hii ajali zilikuwa nyingi sana katika maeneo ya kazi na wafanyakazi wengi sana walikuwa wanapata ulemavu. Lakini kwasasa baada ya kutoa elimu, maelekezo na ushauri na baada ya kuwa karibu na wenye viwanda na wafanyakazi, ajali zimepunguwa kwa kiwango kikubwa sana na wenyewe wamejua sasa umuhimu wa kuzingatia ushauri na maelekezo yanayotolewa na Mamlaka,” amesema Sanga.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amesema shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda zinakuwa kwa kasi katika wilaya yake hivyo kupelekea umuhimu wa ofisi yake kushirikiana kwa karibu na OSHA katika kulea shughuli hizo za kiuchumi ili ziweze kukuwa na kuleta tija.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amemshukuru Mkuu wa Wilaya huyo kwa kutambua mchango wa taasisi yake katika kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Mkuranga na Taifa kwa ujumla.
“Tumepata heshima kubwa kutembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Filbert Sanga, ambaye nia na madhumuni ya ziara yake hapa kwetu ni kutaka kujua ni namna gani sisi (OSHA) tunatekeleza majukumu yetu. Tumejadiliana nae mambo mengi kuhusiana na kulinda rasilimali watu katika wilaya yake ambayo ina viwanda na shughuli nyingi za kiuchumi,” amesema Mwenda na kuongeza:
“Kimsingi ameona taasisi ya OSHA inamchango mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba eneo lake linaendelea kukua kiuchumi kwasababu wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunalinda nguvukazi lakini pia tunalinda mtaji wa mwekezaji kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija. Tunamuahidi Mhe. Mkuu wa Wilaya pamoja na wadau wengine kwamba tutaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria kwa kutoa miongozo na ushauri ili kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi yanakuwa salama wakati wote,”.
Awali, viongozi hao wawili walikuwa na kikao kifupi ambapo walibadilishana mawazo juu ya namna ambavyo taasisi ya OSHA inaweza kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi katika wilaya hiyo yenye viwanda vikubwa zaidi ya 90 pamoja na shughuli nyinginezo nyingi za kiuchumi.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu yenye jukumu la kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama ili kuepuka ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.