32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

DC Jokate kuandaa wanawake wenye elimu

Na CHRISTINA GAULUHANGA-KISARAWE

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani , Jokate Mwegelo, amesema amejipanga kuhakikisha  anaandaa wanawake shupavu wenye weledi na elimu ya kutosha ambao watachochea uchumi wa nchi kukua.

Akizungumza na waandishi wa habari   mjini Kisarawe jana kuhusu harambee ya Tokomeza Zero Kisarawe ambayo ilifanyika Machi 30, mwaka huu,  alisema  ameamua kujenga shule ya sekondari ya bweni ambayo itakuwa ya mfano.

Alisema lengo   kubwa ni kuhakikisha  anainua kiwango cha elimu ndani ya wilaya hiyo   na kuboresha miundombinu ya shule na kujenga mazingira bora ya kufundishia.

“’Tumeazimia kujenga shule ya bweni ya watoto wa kike na kiume lakini kipaumbele chetu ni watoto wa kike  kwa sababu  sote tunafahamu changamoto walizonazo,” alisema Jokate.

Alisema hadi sasa katika harambee hiyo zimekusanywa  zaidi ya Sh milioni 900 ambazo zitatumika shule itakayokuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita.

Jokate alisema  katika harambee iliyoifanya Machi 30, mwaka huu yenye lengo ya kukusanya fedha za ujenzi wa shule hiyo iliyo Kata ya Kibuta Kijiji cha Muhaga, Kisarawe zilipokewa fedha taslimu Sh milioni 80 ambazo zipo tayari benki na ahadi.

“Kama wilaya mwaka huu tulikataa kusherehekea sikukuu ya wanawake inayofanyika kila mwaka Machi 8, na badala yake tukaamua kuendesha harambee hii, tunashukuru imefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Jokate.

Alisema matarajio yao shule hiyo iwe imekamilika hadi ifikapo Septemba mwaka huu.

Alisema  awali liliwekwa lengo la kukusanya Sh bilioni 1.3  na  imani ni kwamba  lengo litafikiwa  kwa sababu ya mwamko wa wadau mbalimbali.

Akielezea historia ya elimu katika wilaya hiyo, alisema  mwaka 2014/2017 watoto waliomaliza kidato cha nne walikuwa 4,880 ambako waliofanikiwa kumaliza kidato cha sita ni 66 tu.

Alisema pia zimepokewa ahadi za vifaa mbalimbali ikiwamo saruji, kokoto, mbao, mabweni, sare za shule, maktaba,  mashine za kusafisha maji,  msaada wa  sheria  na ujenzi wa miundombinu ya walemavu.

Alisisitiza kuwa wilaya hiyo ina rasilimali za kutosha hivyo  atahakikisha  anatengeneza miundombinu wezeshi itakayosaidia wananchi wa wilaya hiyo kujikomboa kwa uchumi na elimu.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe, Mussa Gama, alisema  mradi huo ulikuwapo tangu awali kilichokuwa kinakwamisha ni fedha.

Aliwashukuru wadau waliochangia mradi huo na kuahidi kutumia fedha na vifaa vilivyotolewa kama ilivyokusudiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles