Na JOHANES RESPICHIUS-PWANI
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameendesha operesheni ya kuondoa wafugaji waliovamia msitu wa Ruvu Kusini mkoani Pwani.
Operesheni hiyo ambayo ilianza jana na kupewa jina la ‘Operesheni Jokate’ ilifanikisha kukamata ng’ombe zaidi ya 150 ambao walikuwa wanachungwa katika msitu huo kinyume cha sheria, ni ya kwanza tangu alipoanza rasmi kazi Agosti 6, mwaka huu.
Akizungumza katika opereshini hiyo, Mwegelo aliwataka wananchi kuacha kufanya shughuli mbalimbali katika hifadhi za misitu na atakayekaidi atachukuliwa hatua za sheria.
“Msitu huu unahifadhiwa kwa mujibu wa sheria namba 14 ya mwaka 2002 ya uhifadhi wa misitu ambayo inazuia shuguli zote za jamii na uchumi kufanyika katika hifadhi za misitu.
“Kwa hiyo tunaondoa mifugo yote na makazi ambayo yapo kwenye hifadhi… kwa hiyo hatutavumilia mwananchi yoyote ambaye atakiuka agizo la serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alilotoa siku ya kupanda miti akitaka shughuli zinazofanyika hifadhi za misitu kusimamishwa mara moja.
“Tuna vijiji zaidi ya 66 lakini vinavyoruhusiwa kwa shughuli za ufugaji ni 24 na hiyo haielekezi kwamba wafugaji wa vijiji hivyo wanaweza kulisha mifugo kwenye msitu, tutawachukulia hatua za sheria,” alisema Mwegelo.
Alisema operesheni hiyo inatarajia kuchukua takribani siku sita na inazihusisha wilaya mbili, Kibaha na Kisarawe na itakuwa endelevu kuhakikisha maeneo ambayo yamehifadhiwa yanaendelea kuwa salama bila kuharibiwa na shuguli za jamii na uchumi.
Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania, Caroline Malundo, alisema msitu huo ni muhimu katika Mkoa wa Pwani kwa sababu unahifadhi vyanzo vya maji, hewa na hali ya mazingira.
Alisema robo ya msitu huo wenye hekta 31,663 imevamiwa kwa shughuli za binadamu hususan ufugaji, kilimo na wachoma mkaa.
Wakati huo huo, DC Mwegelo alishiriki kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyoshaji ambako aliwataka viongozi katika ngazi zote wilaya hiyo kuhamasisha na kutoa elimu ya kunyonyesha watoto.
Vilevile, aliwataka waajiri kuwapa ruhusu ya saa mbili kila siku wanawake wanaonyonyesha katika kipindi cha miezi sita.
“Suala la unyonyeshaji siyo la mama peke yao, hata baba anapaswa kushiriki kwa ukamilifu hasa katika kuhakikisha mama anayenyonyesha anapata lishe bora kumwezesha kupata maziwa ya kutosha,” alisema.
Meneja Programu wa Chakula na Lishe kutoka Taasisi ya Feed Children, Sylvia Imalike, alishauri kina mama kuacha tabia ya kuwapa maji watoto wakiwa chini ya miezi sita.
Alisema maziwa ya mama yana zaidi ya asilimia 80 ya maji hivyo wanapaswa kufuata ushauri wanaopewa na madaktari.