24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC Ileje awataka walimu kuwa wazalendo

Na Denis Sikonde, Songwe

Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya amewataka walimu wilayani humo kuwa wazalendo ikiwemo kusimamia taaluma yao kwa kuzalisha kizazi ambacho ni viongozi wa taifa la kesho.

Sehemu ya washiriki.

Gidarya ametoa rai hiyo Septemba 28, 2022 katika hafla ya uzinduzi wa miongozo mitatu ya usimamizi na uendeshaji wa elimu uliofanyika katika shule ya sekondari Itumba ukihudhuriwa na wadau wa elimu kutoka kata 18 za wilaya hiyo.

Kikao hicho kilihusisha walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, waratibu elimu kata, madiwani pamoja na wakuu wa idara na vitengo.

Akizungumza kabla ya kuzindua miongozo hiyo, Gidarya amewaagiza wasimamizi wa elimu kusimamia na kuondoa changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutomudu stadi za Kuandika, Kuhesabu na Kusoma (KKK).

“Mkaondoe udhaifu wa baadhi ya viongozi katika usimamizi na ufuatiliaji, pamoja na kuacha kutoa vitisho kwa walimu pindi wanapotekeleza majukumu yao kufundisha na kuwadhibu wanafunzi watoro,” amesema Gidarya.

Aidha, Gidarya amewataka madiwani kuacha kutumia siasa kwenye usimamizi wa elimu bali washirikiane na walimu kwenye maeneo yao kwa kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa elimu na wazazi watakaokaidi wachukuliwe hatua za kisheria.

“Hakikisheni mnawachukulia hatua wazazi na walezi watakaokataa kuwapeleka watoto shule ili kila mtoto apate haki ya msingi sambamba na kudhibiti utoro kwa wanafunzi,” amesema Gidarya.

Akizungumza kwaniaba ya madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ubatizo Songa amesema miongozo hiyo itasaidia kuandaa kizazi ambacho kitakuwa na elimu itakayolisaidia taifa, huku ufuatiliaji wa ufundishaji kwa walimu kila mwezi huku akitaka ufanyiwe kazi ili kubaini uwajibikaji hafifu kwa baadhi ya walimu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pastory Mashiku amesema maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya yatafanyiwa kazi, kwa kuwataka wakuu wa idara ya msingi na sekondari kwa kushirikiana na wataalamu ngazi ya kata kusimamia miongozo hiyo ili ilete tija kwa wilaya ya Ileje.

Miongozo hiyo mitatu imeundwa Julai, mwaka huu kupitia Wizara ya TAMISEMI ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya sita kuboresha elimu ili wananchi wake wapate elimu bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles