27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

DC Ileje atatua mgogoro wa maji vijiji vya Kapeta na Lema Kyela

*Wananchi waahidi kuulinda kwa imani za kichifu ili udumu kwa miaka 20

Na Denis Sikonde, Songwe

Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya na Mkuu wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, SACP Ismail Mlawa wamemaliza utata wa wananchi wa kijiji cha Kapeta wilaya ya ILeje kukatalia wananchi wa kijiji cha Lema wilaya ya Kyela kuvuta maji kutoka Kapeta wakihofia chanzo hicho kukauka.

Viongozi hao wa wilaya hizo jirani wamefanikisha kumaliza utata huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Alhamisi Februari 10, 2022 katika Kijiji cha Kapeta ambao umehusisha viongozi kutoka Ileje wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Anna Gidarya na wataalamu kutoka wilaya ya Kyela wakiongozwa pia na Mkuu wa wilaya hiyo, SACP Ismail Mlawa.

DC Gidarya amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inatatua kero ya wananchi ya kukosa maji safi na salama na kuwataka wananchi wa kushirikiana kulinda vyanzo vya maji kwa pande zote za Kyela na Ileje ili chanzo hicho kitumike kwa muda mrefu.

“Pindi wananchi wa Lema watakapotumia chanzo hicho kupata maji safi na salama wasiharibu miundombinu, kwani rasilimali zote ni miliki ya wa Tanzania hivyo kukubali kwao kutaendeleza uhusiano mzuri baina ya vijiji hivyo jirani vya Kapeta kilichopo kata ya Ikinga wilaya ya Ileje na kijiji cha Lema kilichopo kata ya Busale wilaya ya Kyela,” amesema Gidarya.

Sehemu ya Wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, SACP Ismail Mlawa, ameushukuru uongozi wa wilaya ya Ileje kwa ushirikiano wa kumaliza utata wa wananchi kutoruhusu wananchi wa Lema kutumia chanzo cha Kapeta kupata maji, hivyo wananchi wa Kapeta wameonyesha ukomavu wa ujirani mwema, hivyo ameahidi kushirikiana kulinda chanzo hicho.

Akizungumza katika mkutano huo Kaimu Meneja wa Walaka wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Ileje, Brighton Paschal amesema kama wataalamu watahakikisha wananchi wa pande zote mbili wanatumia chanzo hicho bila kuathiri mradi wa awali uliko katika kijiji cha Kapeta uliogharumu Sh milioni 190.

Mradi huo uliokamilika mwaka 2018 unahudumia wananchi 1,504.

Upande wake Meneja wa RUWASA wilaya ya Kyela, Mhandisi Tanu Deule amesema wao kama wataalamu watahakikisha wanashirikiana kulinda miundombinu ya maji sambamba na kulinda vyanzo vya maji na kuwasihi wananchi kuepuka shughuli za binadamu karibu na vyanzo vya maji.

Mkuu wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, SACP Ismail Mlawa.

Kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Kapeta wamesema kutokana na kutojua kazi ya utaalamu wa maji kuliwapelekea hofu ya kuathiri huduma ya maji kijijini hapo, hivyo baadaya kupatiwa elimu wamekubali kijiji cha Lema kupata maji huku wakiahidi kulinda mradi huo kwa imani za kichifu ili udumu kwa miaka zaidi ya 20.

Utata wa wananchi wa Kijiji cha Kapeta ulitokea baada ya wataalamu kutoka pande zote mbili kukubaliana kutumia chanzo kilichopo Kapeta kuwahudumia wananchi wa Lema kata ya Busale wilayani Kyela hatua uliyozua mvutano ambao hatimaye umetatuliwa na serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles