Na Brighter Masaki, Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Godwin Gondwe, ametoa siku 14 kwa Mzabuni wa vifaa tiba Bahari Phamacy kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana ndani ya siku 14 kuanzia leo Februari 12.
Sambamba na hilo amemtaka Mzabuni wa Samani katika Hospitali hiyo ambaye ni (Jaffery Industries) hadi kufikia Machi 16, mwaka huu awe ameweka samani zote kwa mujibu wa mkataba katika kituo hicho cha Afya kilichoko wilani humo.
Ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Februari 12, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Kituo hicho cha Afya cha kisasa, mradi unaotekelezwa na Mradi wa uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam(DMDP).
Akiwa katika kituo hicho cha Afya, Gondwe alipata wasaa wa kukikagua na kupata taarifa ya gharama ya ujenzi wa kituo hicho ambapo hadi kukamilika kwake kitagharimu Sh bilioni 4.4.
Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Gwamaka Mwabukambo, omeeleza kuwa katika fedha hizo Sh bilioni 2.2 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo na Sh bilioni 2.2 ni kwa ajili ya vifaa tiba na samani,
“Wananchi wa Buza wanataka kuona kituo cha Afya kinafanya kazi hivyo lazima kazi zifanyike kwa kuzingatia mkataba na kazi zikamilike kwa wakati,” amesema Gondwe.
Ifahamike kuwa Kata ya Buza pekee ina miradi yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 18 ambayo inatekelezwa na DMDPikiwa ni pamoja na Kituo cha Afya na miradi mingine ya barabara.
Aidha, katika ziara hiyo Gondwe aliambatana na kamati ya Ulinzi na Usalama, Katibu Tawala wa Wilaya pamoja na Wataalamu kutoka Manipaa ya Temeke.