MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, amebaini kuwapo hati za makazi feki zaidi ya 140 zilizotolewa na watendaji kinyume cha utaratibu na kusababisha migogoro ya ardhi.
Alisema hayo juzi baada ya kukagua mipaka ya Shule ya Msingi Seuta na kubaini kuuzwa eneo la shule hiyo kwa mwananchi kinyume cha utaratibu.
Gondwe alisema katika hati 150 za umiliki zilizofikishwa na wananchi katika ofisi yake, ni 10 pekee ndiyo halali, huku zilizobaki 140 zikiwa zimegushiwa.
“Natoa siku 14 kwa maofisa wa ardhi wilayani hapa kuhakikisha wanayapitia maeneo yote yenye migogoro na kuweza kubaini waliohusika na uuzwaji wa maeneo na kutoa hati bandia kwa wananchi,” alisema Gondwe.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha migogoro mingi ndani ya wilaya hiyo imesababishwa na watendaji wasio waaminifu, ambao wapo kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe na si kusaidia Serikali.
Gondwe alisema atahakikisha maeneo yote yaliyouzwa kinyume cha utaratibu kwa wananchi yanarudi mikononi mwa Serikali na waliohusika wanachukuliwa hatua stahiki.
“Nitahakikisha maeneo yote ya wazi na yale ya Serikali yaliyovamiwa nayarudisha mikononi kwa umiliki wa Serikali na waliohusika nitawafikisha kwenye vyombo vinavyohusika,” alisema Gondwe.