31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kwanini Uganda na si Tanzania?

Cranes-fansNA ERNEST CHENGELELA (OUT)

KWANINI Uganda na si Tanzania? Ni swali ambalo wadau wa soka nchini wamekuwa wakijiuliza mara baada ya The Cranes kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017, huku Taifa Stars ikiburuza mkia kwenye kundi lake.

Unaweza kujiuliza je, ni wapi Tanzania kama nchi imekosea? Je, Uganda imewezaje kuvunja mwiko wa miaka 38 na kwenda Gabon, wakati Taifa Stars ikiendelea kusubiri tangu mwaka 1980? Inasikitisha sana!

Inawezekana Uganda wamejiuliza maswali sahihi ambayo yamewapa majibu sahihi ya wapi walikuwa wanakosea, hatimaye wamefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki Afcon kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978.

Kitu ambacho Tanzania imeshindwa kufanya zaidi ya kuendeleza siasa na zengwe, ambalo mwisho wa siku limeifanya nchi kila kukicha kupiga hatua mbili mbele na kurudi nyuma hatua 10 huku ikijipongeza.

Hadi leo hii kwanini kama nchi watu hawajiulizi sababu za msingi za michezo ya shule za msingi (Umitashumta) na sekondari (Umiseta) kufutwa? Kwanini watu hawajiulizi sababu zilizosababisha Kim Poulsen kutimuliwa Taifa Stars? Kwanini hakuna anayejiuliza kwanini amerudishwa? Inashangaza sana!

Kwanini hakuna anayewaambia Watanzania mchango wa Kim Poulsen kwenye mafanikio ya Serengeti Boys kwa sasa? Kitendo cha kushindwa kujiuliza maswali haya ya msingi ndicho kinachosababisha nchi iendelee kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ miaka nenda rudi.

Kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisingemtimua Poulsen, si ajabu Taifa Stars ingekuwa inaongozana na Uganda kwenda Afcon 2017 nchini Gabon, lakini hilo limeshindikana kwa sababu hata waliyemtimua hawakujua sababu za kufanya hivyo ndiyo maana wamemrudisha.

Tangu alipopewa Serengeti Boys kwa mara ya kwanza, Poulsen alionyesha mwanga wa kutengeneza timu kwa ajili ya kuja kuitoa Tanzania shimoni na matunda yake ni wachezaji kama akina Frank Domayo, Aboubakar Salum ‘Sure Boy’ na wengine.

Alivyopandishwa Taifa Stars alipanda na wachezaji hawa ambao alionekana kutengeneza timu ya kuibeba nchi kupitia kwao, lakini cha ajabu alifungishwa virago bila hata kuangalia kuwa uwepo wake ungeweza kulipeleka Taifa Afcon mwaka 2017.

Moja ya utetezi wa ‘kipuuzi’ juu ya kuendelea kufeli kwa Tanzania kushiriki Afcon, ni kwasababu kuwa nchi haina wachezaji wengi wa kutosha kwenye ligi za nje, lakini vipi kuhusu ubora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara? Mbona inazifunika ligi nyingi katika ukanda wa  Afrika Mashariki.

Angalia kikosi cha Uganda kilichofuzu kushiriki Afcon, kilikuwa na watu wangapi ambao wamepita kwenye VPL, beki wao tegemeo, Jjuuko Murshid yuko Simba, staa kama Emmanuel Okwi amepita Simba, Hamis Kiiza ambaye alikuwepo kwenye baadhi ya mechi za awali za kundi lao naye amepita Simba na Yanga.

Kocha wa Uganda Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’, naye amewahi kupita Tanzania akifundisha klabu ya Yanga, sasa kama VPL ni mbovu mbona ina wachezaji wengi ambao wanaweza kuzibeba timu zao za Taifa kama ambavyo Vincent Bossou wa Yanga ameibeba Togo.

Hivyo mafanikio ya wachezaji hawa ambao wanaaminiwa kwenye timu zao za Taifa ni ushahidi tosha kuwa VPL ni ligi bora na si tatizo la Taifa Stars kufanya vibaya kila kukicha kwenye michuano ya kimataifa, bali tatizo ni mfumo mzima wa soka la Tanzania ambalo kwa kiasi kikubwa limeendekeza siasa na mizengwe kuliko mipango ya maendeleo.

NINI KIFANYIKE?

Kitendo cha kushindwa kujiuliza maswali sahihi ndicho kimeendelea kuleta majibu mabovu juu ya tatizo la soka la Tanzania kimataifa, hivyo badala ya kuendelea kulaumu ni wakati wa kujiuliza nini kifanyike ili Tanzania ifuate nyayo za Uganda kwenye michuano ijayo ya kimataifa.

Kwanza Serikali inatakiwa kurudisha michezo shuleni na kuifanya iwe ya lazima kama ambavyo Kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Iddi Kipingu, amefanya katika shule yake ya Lord Baden Powel iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam.

Uganda imefanikiwa kuzalisha wachezaji wengi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kutokana na kuwekeza kwenye michezo shuleni, hivyo ni wakati wa Tanzania kurudisha nguvu kwenye michezo shuleni ili kutengeneza timu ya taifa yenye ushindani zaidi siku za usoni.

Lakini mbali na michezo kurudishwa, TFF inatakiwa kuwekeza kwenye soka la vijana kwa kuwaanzishia ligi yenye ushindani na pia kuzibana klabu zote kuwa na shule za soka kwa sababu kwa kufanya hivyo kutaongeza uwezekano wa kukuza na kulea vipaji vitakavyokuja kulibeba Taifa katika siku za usoni.

Pia TFF inatakiwa kuzalisha makocha wengi zaidi wenye viwango vya kimataifa ambao watatengeneza msingi wa soka la Tanzania kwa kulea vijana ambao watakuja kulibeba Taifa siku za usoni.

TFF inatakiwa kutambua kuwa Watanzania wamechoka kusherehekea mafanikio ya timu nyingine na huu ni wakati wao mwafaka wa kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha Taifa Stars inashiriki kwenye Afcon mwaka 2019.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles