Na SAMWEL MWANGA
MKUU wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe amewataka
madaktari na wauguzi katika hospitali ya wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya kazi zao.
Alitoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari baada ya kutembelea hospitali ya wilaya hiyo na kujionea
changamoto zinazoikabili.
DC alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo upungufu wa vifaa tiba na dawa.
Alisema watumishi wa hospitali hiyo pia hawawajibiki ipasavyo hivyo kusababisha wagonjwa kutopata huduma bora
za afya.
Mkuu huyo wa wilaya alisema licha ya kukabiliwa changamoto hizo, hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kuonyesha upendo na upole kwa wagonjwa kwa kutoa huduma bora.
Alisema huduma hiyo iwe ni pamoja na kuwaelimisha
watumiaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii wanapofika kutibiwa hospitalini hapo.
“Zipo changamoto zinazoikabili hospitali yetu ya Wilaya ya Maswa pia wapo wananchi wetu ambao ni wagonjwa waliojiunga na mifuko ya bima ya afya na mfuko wa afya ya jamii kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Lakini wanapofika katika hospitali yetu hawapatiwi elimu juu ya huduma wanazopaswa kuhudumiwa na wakati mwingine hujikuta wanalipia matibabu mara mbili jambo ambalo si zuri,” alisema.
Alimwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Vedastus Luguga kuwachukulia hatua kali za nidhamu na kuhakikisha anasimamia suala la kutolewa huduma bora
za afya kwa wagonjwa.
Alisema serikali wilayani humo imejipanga kukabiliana na
changamoto za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kuanzisha duka kubwa la dawa ndani ya hospitali hiyo.
“Hii ni hospitali kubwa na inatoa huduma hadi kwa baadhi ya wananchi wa wilaya jirani za Itilima na Meatu mkoani Simiyu na wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambazo zinapakana na wilaya ya Maswa,” alisema.