31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DC aunda kamati kuchunguza mgomo

novatusNa Safina Sarwatt, Moshi

MKUU wa Wilaya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Novatus Makunga ameunda kamati tatu ya kuchunguza mgomo  baridi  wa madakatari na manesi  unaendelea katika  Hospitali ya Kibosho, wakipinga lugha chafu, ubabe unaofanywa na uongozi wa hospitali hiyo na  kucheleweshewa mishahara.

Hatua hiyo ya mkuu huyo kuunda tume imekuja mara baada ya kufanya kikao na watumishi, kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya wagonjwa kuhusu huduma mbovu.

Akitoa agizo la kuundwa kwa kamati tatu za kiuchunguzi, Makunga alisema sekta ya afya ni eneo ambalo halitakiwi kufanyiwa mzaha hata kidogo na kumtaka mganga mkuu wa halmashauri kutolea ufafanuzi madai hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, watumishi hao wamekuwa wakituhumu uongozi wa hospitali hiyo kuwaendesha kibabe, huku  wakidai kutolipwa mishahara na kufanyakazi bila mapumziko.

“Mishahara tunacheleweshewa  tunatembea umbali mrefu hakuna nyumba za watumishi, nyumba zilizopo zimetolewa kwa upendeleo kwa baadhi ya watumishi, tunafanyakazi katika mazingira magumu sana, hakuna posho kwa ajili ya saa za nyogeza kazini,” alisema muuguzi mmoja.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. John Materu, alisema kuwa hakuna tatizo la ucheleweshwaji wa mishahara wala upendeleo katika kutoa nyumba kwa watumishi na kwamba nyumba chache zilizopo walipewa madaktari bingwa.

Alisema kuwa malalamiko hayo hayana msingi yoyote ambapo alidai hali hiyo ilikuja mara tu baada ya uongozi wa hospitali kuboresha utoaji wa huduma na kuweka usimamizi  katika kitengo cha ukusanyaji wa mapato ya hospitali.

Alisema madaktari walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea ambapo wagonjwa walikuwa wakikaa katika foleni kwa muda mrefu kusubiria kuingia kwa daktari.

“Baada ya uongozi kupiga vita uzembe kazini tuliweza kutokomeza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi ambapo kwa kipindi cha mwaka juzi wajawazito 4,000 walijifungua salama,”alisema.

Dk. Materu alisema hospitali hiyo inawatumishi walioko chini ya Serikali  na watumishi walioko chini ya hospitali na kwamba watumishi walioko chini ya hospitali hakuna anayedai mishahara wala fedha za kuitwa kazini  wakati wa dharura.

Alisema kulingana na kasi ya Rais  Dk. John Magufuli  ni lazima mifumo ya utendaji wa kazi ibadilike. “Tuache uzembe kazini lengo hapa ni kuboresha utoaji wa huduma kwa Watanzania,” alisema.

Katika hatua nyingine alisema kuwa hospitali hiyo imeweza kukusanya zaidi za bilioni moja na fedha nyingine zilielekezwa katika ununuzi wa vifaa vya kisasa na dawa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles