Tunu Nassor, Dar es Salaam
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) imewashauri wakazi wa Temeke kutumia mradi mpya wa kuchakata majitaka uliozinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva pindi wanapotaka kunyonya vyoo vyao.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Jamii wa Dawasa, Neli Msuya amesema mradi huo utawapunguzia gharama za unyonyaji majitaka kwa wakazi wa kaya zisizopangwa.
“Niwaombe wananchi mtumie mradi huu mnapokuwa na uhitaji wa kunyonya vyoo vyenu kwa kuwa utakuwa na gharama nafuu huku ukiyaacha mazingira yakiwa safi,” amesema Neli.
Amewaomba wakazi wa kata nyingine za jiji la Dar es Salaam kupokea na kushiriki katika miradi ya majitaka itakayopelekwa kwao na serikali.
“Dawasa inawashukuru wakazi wa Miburani kwa kupokea mradi huu hivyo tunawaomba mitaa mingine waige mfano huu nao wapokee miradi mingine ya serikali itakayopelekwa,” amesema Neli.
Aidha amewataka kuwekeza fedha kidogo kidogo ili kuwasaidia wanapokuwa na uhitaji wa kunyonya vyoo vyao.
Kwa upande wake Mhandisi wa Manispaa ya Temeke, Primy Damas amesema mradi huo umegharimu Sh Milioni 120.
Amesema mradi utakuwa na uwezo wa kuchakata majitaka lita 10,000 kwa siku na utahusisha unyonyaji, usafirishaji na uchakataji wa majitaka.
“Kuanza kwa mradi huu kutapunguza changamoto ya utunzaji majitaka katika maeneo yasiyopangwa ambayo huleta athari za mazingira na madhara ya afya za wanadamu,” amesema Damasi.
Naye Ofisa Tarafa wa Chang’ombe Aimbora Nnko amewataka wakazi wa kata hiyo kuwa walinzi wa mradi huo.
“Niwaombe mfuatilie na kuwakamata wale wanaotapisha vyoo kipindi cha mvua na kuwaadhibu kulingana na sheria,” amesema Aimbora.