27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

DAWA ZA KULEVYA ZAZUA MAPYA DAR

AZIZA MASOUD na ASHA BANI 

-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwataja kwa majina askari polisi na wasanii wakiwamo wale wenye majina makubwa katika sakata la dawa za kulevya, jana kiongozi huyo amewaongeza kwenye orodha hiyo mwanamuziki, Vanessa  Mdee, mrembo anayependezesha video za muziki, Tunda na askari wengine watano.

Pamoja na Vanessa na Tunda, watu wengine wanne wametakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Jumatatu kujieleza baada ya kutuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya kama ilivyokuwa kwa wasanii wengine waliotajwa juzi.

Mbali na hilo, Makonda pia ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwaweka ndani mpaka Jumatatu kwa ajili ya kutoa maelezo watu wote wakiwemo wasanii walioshindwa kuripoti jana.

Walioitika wito wa Mkuu huyo wa mkoa jana kwa kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi ni pamoja na Wema Sepetu, Hamidu Changuso ‘Dogo Hamidu’, Khalid Mohamed ‘TID’ na Babu wa Kitaa.

Wasanii ambao hawakuitika wito wa Mkuu huyo wa mkoa ni pamoja na Rachel, Sniper, Tito, Chid Benz na Heri Samir (Mr Blue) ambaye inasemekana yupo Uarabuni. 

Makonda na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, wakizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Kituo hicho kabla ya kuelekea Ikulu waliokoitwa na Rais Dk. John Magufuli, walisema kuhojiwa kwa watu hao kunaweza kuchangia kufanikisha kukamata wasambazaji pamoja na waingizaji wa dawa za kulevya nchini.

“Jumatatu wanaopaswa kuwepo ni Omari Sanga, Kashozi, Amani, Halidali Katwila, Tunda hawa wote nawahitaji Jumatatu hapa Central (Kituo cha Kati) akiweno dada yangu kipenzi, Vanessa  sisi tunaanza na hawa wanaotumia itatusaidia,” alisema Makonda.

Alisema taarifa alizonazo, Sanga ni mmoja kati ya watu waliosababisha si chini ya Watanzania asilimia 65 au 70 kufungwa katika magereza yaliyopo China.

“Sasa hivi yupo Dubai anaprocess (anafanya taratibu) kwenda China lakini mkono wa Mungu ni mkubwa na mkono wa Serikali ya Magufuli mkubwa tutamdaka tu.

“Huyu mtu si muda mrefu mwezi mmoja uliopita alikuwa kwenye hoteli moja hapa Sinza kasambaza mzigo wake mpaka kamaliza ndiyo kaondoka, anaweza kukaa hotelini hata wiki mbili tatu ndiyo anaondoka,” alisema Makonda.

Alisema ofisi yake imekwishawasiliana na vyombo mbalimbali ikiwemo Idara ya Uhamiaji na Uwanja wa Ndege ili  kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa.

“Kuwahoji hawa itatusaidia mambo mawili, kuna mwingine anasema ameacha lakini anasema hakumbuki alipochukua, basi kama unatumia unajua yanapouzwa, kama hujui unapata wapi maana yake wewe unatengeneza dawa, ukitengeneza dawa ukaitumia mwenyewe haina shida ukiisambaza tunakutafuta,” alisema Makonda.

Mbali na watu hao, Makonda pia aliitaja hoteli moja kubwa iliyopo jijini Dar es Salaam ambayo ina chumba maalumu kwa ajili ya kuvutia dawa hizo.

“Kuna hoteli moja ipo pale nyuma ya nyumba za National Housing za Kawe inaitwa sijui Meditarian ipo baharini kabisa mmiliki wake anaitwa Samantha Mgiriki, nimepata taarifa ‘swimming pool’ yake inatumiwa vizuri sana na baadhi ya vijana kuburudika na kuna vyumba pia maalumu kwa ajili ya kuburudika,” alisema Makonda.

Makonda pia alisema katika uchunguzi wake amebaini uwepo wa askari wengine watano mbali na wale 10 aliotangaza juzi wakituhumiwa kusaidia biashara ya dawa za kulevya.

Alisema katika orodha hiyo wapo ambao katika wiki za hivi karibuni wamepatiwa Sh bilioni moja ili kuwalinda wafanyabiashara hao.

Katika orodha hiyo mpya, Makonda hata hivyo aliwataja kwa majina askari watatu tu ambao ni Mudy Zungu, Fadhili na Ben.

“Hawa watatu uwaunganishe kwenye ile timu nyingine yako kuhakikisha unashughulika nao, kuna mwingine  amenunua nyumba Kigamboni na fedha hizi za dawa za kulevya,” alimweleza Kamanda Sirro na kuongeza:

“Kamanda Sirro tukishashinda hii vita tutakula kuku kama si hapa duniani basi hata mbinguni.”

Alisema lengo la operesheni hiyo ni  kurudisha heshima ya Taifa na waasisi wake wakiwemo Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

“Ukienda baadhi ya nchi ukionyesha passport (hati ya kusafiria) tu ikionyesha Tanzania unaonekana umebeba dawa za kulevya,” alisema Makonda.

Alisema lengo la kukutana na watu hao  ni kutaka wawapatie taarifa za wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na baadaye wazifanyie kazi.

“Vita hii haiishi leo inaisha pale ambapo madawa yameisha, vita hii si ya Kamanda Sirro, si ya Rais Magufuli wala si ya Makonda, ni vita ya kila mtu anayekaa Dar es Salaam, hawa watu tunaishi nao tunacheza nao na wengine ni wafadhili wetu, ni wakati wa kuwatoa hadharani ili watoto wetu na Taifa letu lipone,” alisema Makonda.

Kwa upande wa Kamanda Sirro, alisema Jeshi hilo kwa sasa limeunda kitengo maalumu cha kushughulikia dawa za kulevya kikiongozwa na watu mbalimbali waliopo ndani ya vyombo vya usalama.

Kuhusu polisi 12 waliotajwa juzi alisema saba tu ndio waliohojiwa, wawili hawajahojiwa kwa sababu walihamishiwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema askari wengine wawili hawajafika kuhojiwa na hivyo kutangaza kuwatafuta.

Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, watu wote waliokamatwa na wanaoendelea kuhojiwa wataachiwa baada ya polisi kujiridhisha.

Awali wasanii, Wema Sepetu,

TID, Dogo Hamidu, Babuu wa Kitaa pamoja na mtu mmoja ambaye jina lake halikupatikana, walifika Kituo cha Kati na kuhojiwa kwa saa kadhaa.

Katika kituo hicho, wasanii hao walikuwa wakiingia kwa awamu ambapo Wema alikuwa msanii wa mwisho kuwasili kituoni hapo akiwa amevaa dera  na mtandio kichwani.

Wema awali alishuka kwenye gari binafsi aina ya Brevis huku akiwa amejifunika usoni na mtandio na hivyo waandishi wa habari kushindwa kumtambua kwa urahisi.

Ndani ya vyumba vya mahojiano ambavyo waandishi wa habari hawakuruhusiwa, sauti ya Wema ilisikika akilia huku polisi wakijaribu kumtia moyo kwamba suala hilo ni kama upepo na utapita.

Sauti hiyo iliwafanya baadhi ya waandishi kukisogelea chumba hicho na kumshuhudia Wema akilia.

Baada ya kuhojiwa, Wema pia aliamuriwa na maofisa hao wa Jeshi la Polisi kwenda katika ofisi ya Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, kwa mahojiano zaidi.

Baada ya kutoka katika chumba hicho alichokuwa awali msanii huyo maarufu nchini alisimama takribani dakika kumi katika korido kabla ya kushuka ngazi,  akiogopa kundi la waandishi na wapiga picha lililokuwa likimsubiri chini.

 

Wema ambaye alikuwa amevaa miwani ya rangi nyeusi, alionekana ni mtu mwenye huzuni alipokuwa akielekea  katika ofisi ya Kamishna Sirro na hadi gazeti hili linakwenda mitamboni saa 3 usiku wasanii wote walikuwa bado wakihojiwa.

Kabla hajakwenda kuhojiwa katika ukurasa wake wa Instagram, Wema alirekodi sauti yake ambayo alisikika akisema:

I thought I should say something (najua ninapaswa kusema kitu) kwa sababu najua I have fans (nina mashabiki) out there I have people look up to me, I have people who love me I have people who  support no matter what I have people who worried about me (nina watu ambao wananiangalia, wananipenda na kunisapoti haijalishi ni nini, nina watu ambao wana wasiwasi) na hawa watu ambao wananijali sana nina uhakika wana wasiwasi sana lakini nataka niwaambie msiwe na wasiwasi.

 

Kwa upande wake TID ambaye aliwasili kituoni hapo saa 5:07 asubuhi, alikuwa amevalia nadhifu huku akitokea eneo kilipo kituo cha mabasi cha Stesheni na kuwaacha watu katika hali ya mshangao  wasijue alitumia usafiri gani.

Dogo Hamidu yeye aliwasili saa 11:37 akiwa amevaa vazi la Kiislamu maarufu kama kanzu pamoja na kofia huku akielekea moja kwa moja katika lango kuu la kituo hicho.

Mtangazaji Babuu wa Kitaa ambaye alikuwa wa kwanza kufika kituoni hapo  saa 4:35 akiwa kwenye gari ndogo, alikuwa ameambatana na mama mmoja ambaye hakushuka kwenye gari.

Tukio hilo lilivuta umati wa watu ambao uliwalazimisha askari kanzu kuwaondoa mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, Kamishna Mihayo Msikhela, alisema hafahamu mazingira ya kutajwa kwa watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya nchini.

Katika maelezo yake kwa gazeti hili, alisema mtu sahihi wa kuulizwa jambo hilo kwa sasa ni Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

“Sijui lolote kuhusiana na hilo na hata mazingira yake siyajui, simjui hata mkubwa anayehusika na uuzaji au usambazaji wa dawa, lakini yote hayo muulize Sirro ambaye ndiye kiongozi wa Dar es Salaam,” alisema Msikhela.

Msikhela aliongeza kwamba suala hilo kwa nchi nzima si rahisi kulifahamu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema wizara yake haifanyi kazi kwa njia ya magazeti.

Masauni ambaye hakupokea simu zaidi ya kutaka kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kutokana na kuwapo kwenye vikao vya Bunge, baada ya kuulizwa kuhusiana na suala hilo na ukubwa wake kitaifa alisema: “Samahani hatuaniki mikakati kwenye gazeti,” alisema Masauni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles