24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA MAMA MJANE PASUA KICHWA

RATIFA BARANYIKWA (DAR)

Na AMINA OMARI-TANGA

SAKATA la ‘mama mjane’ kutoka mkoani Tanga, Swabaha Mohamed Ali, aliyeibuka mbele ya Rais Dk. John Magufuli wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria na kulalamika kudhulumiwa haki yake ya mirathi, limeanza kuchukua sura mpya.

Kwa nyakati tofauti jana, MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na pande mbili zinazovutana katika sakata hilo la mirathi kabla ya baadaye kufika yalikokuwa  makazi ya marehemu, Shosi Mohamed ambaye Swabaha anadai kuwa ni mume wake mkoani Tanga.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi muda mfupi baada ya kusambaa kwa andiko linaloeleza upande wa pili wa ‘mama huyo mjane’ likimtuhumu kama tapeli ambalo limeandikwa na rafiki wa karibu wa familia hiyo, mtoto wa marehemu Shosi aitwae Saburia, alisema madai yote yaliyotolewa na mama huyo mjane si ya kweli na hivyo kutamani Rais Magufuli asikilize upande wa pili unaotuhumiwa wa familia hiyo.

Saburia ambaye alizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu na baadaye nyumbani kwao Tanga, alianza kueleza jinsi anavyomfahamu mama huyo mjane akisema ni dada yake na kwamba marehemu baba yake alikuwa akimwita mjomba.

“Simfahamu kama mke wa marehemu baba, namfahamu kama dada, mama yake mzazi na baba yangu (Shosi) ni mtoto wa mkubwa na mdogo na kwa kabila letu Wagunya aliyepaswa kuolewa na baba yangu ni mama yake ambaye ni shangazi yangu na si yeye.”

Saburia ambaye anajitambulisha kama ndiye msimamizi wa mirathi, anasema baba yake alioa wake watatu ambao ni Mariam Juma Taibu ambaye ni mama yake mzazi aliyekuwa amezaa watoto saba lakini waliohai ni wanne, Mariam Sadick anayeishi Mkumbara Korogwe na Mercy Mwanga ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Kwa kifupi sisi tulikuwa hatumfahamu kabisa, tulimfahamu siku ya 40 baada ya baba kufariki na alikuwa amekuja kutupa pole tukiambiwa kuwa ni ndugu yetu kutoka Mombasa sasa wakati tunaandaa muhtasari wa kikao tukashangaa anasema aliolewa na baba yetu,” anasema.

Kwa mujibu wa Saburia, mama huyo licha ya kudai pia amezaa na baba yao lakini amekuwa akikataa watoto hao wachukuliwe vipimo vya vinasaba (DNA).

Kuhusu kesi, alisema ile ya msingi hadi sasa ipo mahakamani na kwamba hukumu yake inatarajiwa kutolewa Februari 20, mwaka huu.

Akielezea mlolongo mzima wa kesi hiyo na hadi ilipofikia, Saburia anasema kwa mara ya kwanza walifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo Desemba 16, 2012 na walishinda.

“Lakini yeye (Swabaha) alikata rufaa Mahakama ya Wilaya mwaka 2016 akifungua kesi ya kuzuia mali za marehemu ambayo nayo tulishinda na mahakama iliamuru niendelee kuwa msimamizi.”

Saburia ambaye ni miongoni mwa watoto tisa wa marehemu Shosi, anasema baada ya hukumu hiyo, Swabaha alifungua kesi ya haraka, Mahakama Kuu chini ya Jaji Haji Bin Haji, kuomba apewe asimamie mirathi ambako nako alishindwa na hivyo Jaji kuamuru irudishwe mahakama ya wilaya ambako wao walishinda na hivyo kutoa fursa ya kukata rufaa kwa yeyote ambaye hakuridhika na uamuzi huo.

“Hivi tunavyozungumza alikwisha kata rufaa na Februari 20, mwaka huu itatolewa hukumu ya kuendelea na hiyo rufaa au kutoendelea nayo, kesi ipo chini ya Jaji Amuri,” alisema Saburia ambaye anadai anazo nyaraka zote na kuongeza:

“Hebu jiulize, anasema baba alimuoa mwaka 1993, mwaka 2011 alikuwa Buguruni, Dar es Salaam, Eda baada ya kufiwa mume wake mwingine aliyekuwa akiishi naye, mwaka 2013 alikuwa anafuatilia mirathi ya huyo mume wake wa Buguruni, sasa mwanamke anawezaje kuolewa na watu wawili kwa wakati mmoja?” alihoji Saburia ambaye alisema anatarajia kuwasili Dar es Salaam leo ili kuanika kila kitu mbele ya waandishi wa habari.

Wakati Saburia akisema hayo, juzi mbele ya Rais Magufuli, mama huyo mjane, Swabaha alieleza jinsi alivyodhulumiwa haki yake ya mirathi katika mahakama moja mkoani Tanga licha ya kuwa na hati ya kiapo ya kisheria inayompa haki hiyo.

Mama huyo mjane alikaririwa pia na vyombo vya habari akidai kuwa Saburia ni mtoto wa nje wa marehemu mume wake na kwamba amekuwa akitumia nguvu yake ya pesa za dawa za kulevya kutaka kumpora haki yake.

Akijibu tuhuma hizo, Saburia alisema biashara pekee anayojishughulisha nayo ni ile ya nguo na vipodozi.

“Amenidhalilisha kwa kiasi kikubwa  kwani sijawahi na wala sitarajii kujihusisha na biashara hiyo, wakati mwingine familia ndio

inanipa sapoti pale ninapokwama,” alisema.

 

NYUMBANI TANGA

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Marium Taibu ambaye anadai kuwa ni mke mkubwa wa marehemu anayeishi jirani na Hospitali ya Rufaa ya Bombo, alisema anamtambua Swabaha kama mtoto wa wifi yake aliyemtaja kwa jina la Faudhati Mohamed.

Nyumba hiyo anayoishi Taibu kila upande unakiri kuwa yalikuwa ni makazi ya marehemu na shughuli zote za maziko zilifanyika hapo.

Kwa mujibu wa Taibu, makazi ya wifi yake huyo (Faudhati) pamoja na familia yake yapo Mombasa nchini Kenya, hivyo  familia inamtambua Swahaba kama ni ndugu na si mke wa marehemu.

“Najua marehemu aliwahi kuoa wake watatu lakini hakuwahi kusema kama ameongeza mke mwingine na kama angekuwa ameolewa tungeweza kujua kwani tungetambulishwa kwake,” alisema Taibu.

Taibu anasema sakata la Swabaha kudai mirathi hiyo lilianza mwaka 2012 wakati wa kikao cha arobaini ya marehemu mumewe wakati wakili wao alipowasilisha nyaraka ya mirathi.

Anasema Swabaha ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho akijitambulisha kama mpwa wa marehemu na baada ya kusomwa wosia wa marehemu aliomba auone kwa ukaribu ili ajiridhishe na kilichoandikwa.

“Alipopewa akasimama na kusema na yeye ni mke halali wa marehemu hivyo anastahili kurithi mali za marehemu kwani na yeye ana haki na kuamua kukimbia na wosia huo,” anasema Taibu.

Anasema walijaribu kumfuatilia kupitia kwa ndugu pamoja na wazazi wake  kuomba arudishe wosio huo lakini badala yake alikataa na kuamua kuwapa kopi.

Anasema ilipofika Desemba, 2012,  Swabaha akaamua kufungua kesi ya kudai mirathi na kuweka zuio la mali zote za marehemu.

Kwa mujibu wa maelezo yake kesi hiyo ilianzia mahakama ya mwanzo ambapo waliweza kumshinda na baadaye ilipopelekwa mahakama za juu waliamua kumweka Saburia ambaye ni binti mkubwa wa marehemu kuwa msimamizi wa kesi hiyo ya mirathi.

 

MAMA MJANE AZIDI KUFUNGUKA

 

MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na mama huyo mjane kwa njia ya simu baada ya kukataa kumwelekeza mwandishi nyumbani kwake kwa madai kuwa usalama wake upo shakani.

Akizungumza na mwandishi wa MTANZANIA Jumamosi, mama huyo licha ya kusema kwamba hadi jana agizo la Rais Magufuli la kutaka apewe ulinzi lilikuwa bado halijafanyiwa kazi, lakini alisema kwa upande wa Mahakama tayari Jaji Kiongozi alimwandikia barua jana asubuhi.

Alisema Jaji Kiongozi amemwelekeza ayafuate majibu yake kwa Jaji Mfawidhi mkoani Tanga.

Mbali na hayo, MTANZANIA Jumamosi pia lilimuuliza mama huyo kuhusu mahusiano ya kifamilia na kama anamfahamu Saburia au alishiriki msiba wa marehemu mume wake.

Katika majibu yake, Swabaha alikiri kumfahamu Saburia akisema ni mtoto wa nje wa mume wake na kwamba yeye ndio mke halali ingawa mume wake alikuwa na wanawake wengi.

Alikiri kuwa ni kweli marehemu Shosi ambaye alikuwa dereva wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo nje ya nchi licha ya kuwa mume wake alikuwa ni mjomba wake kwa maana mama yake na baba wa Shosi ni mtoto wa mkubwa na mdogo, jambo alilosema kwao si dhambi.

Kuhusu mazishi ya mume wake alikiri kutohudhuria akidai kuwa akina Saburia waliupeleka msiba huo haraka tena bila kuutangaza.

“Sikuwepo ni kweli alifia Bombo lakini sikuwepo, lakini kwenye tatu nilikuwepo na hata arobaini,” alisema huku akimtaka mwandishi amtafute tena baada ya saa moja kupita kisha akakata simu.

Baada ya saa moja kupita mwandishi alimpigia simu tena na miongoni mwa maswali aliyotaka kumuuliza ni pamoja na kutaka kufahamu mwaka ambao Shosi alimuoa, mahali alikokuwa akiishi naye, tuhuma za ndoa ya Buguruni na kama atakuwa tayari kuruhusu DNA ifanyike kwa watoto anaodai kuzaa na marehemu Shosi.

Hata hivyo, mama huyo alimtaka mwandishi awasiliane na Ahmed Shosi ambaye ni mdogo wa marehemu Shosi ili aweze kujibu maswali yote kwa niaba yake kwa kuwa tayari Rais Magufuli alikuwa amewaweka watu kwa ajili ya kufuatilia jambo lake hilo.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Ahmed Shosi ambaye alikiri kumtambua Swabaha kama mke pekee halali wa marehemu kaka yake.

Alisema Swabaha na kaka yake walifunga ndoa mwaka 1993 na kwamba wanawake wengine wote wanaojitokeza kudai kuwa wake za marehemu ni waongo.

Alisema marehemu kaka yake aliwahi kuishi na mama yake Saburia lakini walitengana.

Kuhusu watoto, alisema kaka yake aliacha watoto 11 na kwamba yupo tayari kuongoza watoto si tu wa Swabaha bali wengine wote kwa ajili ya kipimo cha DNA.

Alipoulizwa kama aliwahi kusikia Swabaha aliolewa Buguruni, Ahmed alikiri hilo na kwa maneno yake mwenyewe anasema: “Nilisikia…hata kama aliishi na mume, lakini ninavyojua mimi Swahaba ndio mke halali kwa sababu hata kaka kabla hajafa kwa sababu alikuwa ni tegemeo la familia aliona Swabaha ndio mtu anayeweza kusimamia mali zake.” 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles