WELLINGTON, NEW ZEALAND
WAZIRI Mkuu wa New Zealand, Bill English, amesema nchi yake inalazimika kutegemea wafanyakazi wahamiaji kwa sababu wenyeji wengi wanashindwa kufuzu vipimo vya dawa za kulevya.
English alitoa kauli hiyo wakati alipoulizwa na wanahabari juu ya sababu za kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji nchini hapa.
Kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita, New Zealand ilipokea wahamiaji 71,300 kwa mwaka huu pekee.
Taifa hilo la Bahari ya Pasifiki, lina wakazi milioni 4.8, huku 140,000 kati yao hawana ajira.
English alisema wengi wa wasiokuwa na ajira ni wale walioshindwa kupita kwenye vipimo vya dawa za kulevya, na hivyo kampuni hulazimika kuajiri wahamiaji wenye uwezo na wasio watumiaji wa mihadarati.
Matokeo ya utafiti yaliyochapishwa mwaka 2012 na Jarida la The Lancet, yanaonyesha kuwa New Zealand na Australia zinaongoza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.