28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dawa kutibu TB sugu yapatikana

MAJARIBIO ya mchanganyiko wa dawa mpya ya kutibu Kifua Kikuu sugu nchini Belarus yameonesha mafanikio baada ya kutibu kabisa wagonjwa wanane kati ya 10.

Kwa mujibu wa matokeo ya majaribio hayo yaliyotangazwa Jumatatu wiki hii, dawa hiyo inayoitwa bedaquiline ikitumika sambamba na nyingine za antiobiotiki iliweza kuponya asilimia 80 ya wagonjwa.

Madaktari katika nchi hiyo, ambayo ina viwango vya juu zaidi vya kifua kikuu sugu, kisichosikia dawa duniani waliwafanyia majaribio wagonjwa hao kwa miezi kadhaa.

Matokao hayo yaliyotoka yalikuwa ya kusisimua: Kati ya wagonjwa 181 waliopewa dawa mpya; 168 walikamilisha dozi na 144 walipona kabisa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kabla ya ujio wa dawa hiyo, ni asilimia 55 tu ya watu wenye kifua kikuu sugu hufanikiwa kupona ugonjwa huo.

Aidha, takriban watu milioni 2.5 waliambukizwa maradhi ya TB barani Afrika mwaka 2016 hii ikiwa ni robo ya visa vipya vya ugonjwa huo kote duniani.

Shirika hilo linasema mataifa saba duniani yalikadiria asilimia 64 ya visa vipya vya TB mwaka 2016, India ikiongoza katika mataifa hayo ikifuatiwa na Indonesia, China, Philippines, Pakistan, Nigeria, na Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa WHO, TB iliua watu milioni 1.7 mwaka 2017, na kufanya maradhi hayo ya kuambukiza kuwa hatari zaidi duniani.

Maradhi hayo yanaua zaidi ya mara tatu zaidi ya malaria kila mwaka na yanahusika na wingi wa vifo vya watu wenye VVU/UKIMWI.

Pamoja na kusababisha kiasi kikubwa cha vifo, TB inapokea moja ya 10 tu ya fedha za utafiti zinazoenda kwa VVU/Ukimwi.

TB sugu haitibiki kwa dawa mbili zilizo maarufu zaidi kwa kutibu ugonjwa huo na wataalamu wanaamini inaendelea kwa kasi duniani kutokana na usimamizi mbaya wa kesi za TB.

Tofauti na wauaji wengine wakubwa kama VVU, TB inatibika lakini inahitaji usimamizi wa miezi sita wa umezaji dozi kila siku.

Katika sehemu nyingi duniani dawa huwa hazitunzwi vyema au kuisha kabla ya matibabu kukamilika na kusababisha usugu wa dawa hasa katika maeneo yenye misongamano kama gerezani na hospitalini.

WHO inasema kwamba usugu wa kifua kikuu umeripotiwa katika nchi 117.

Tofauti na dawa nyingine nyingi za antibiotics, bedaquiline haishambulii bakteria moja kwa moja bali hulenga vimeng’enya ambavyo maradhi huvitegemea kupata nishati.

Wagonjwa wote waliofanyiwa majaribio walikutana na athari ndogo ndogo ambazo hata hivyo hazikuwa kali kama ilivyofikiriwa awali.

Mkurugenzi wa Sayansi wa Muungano wa Kupambana na Maradhi ya Kifua Kikuu na Mapafu (The Union), Dk. Paula Fujiwara, anasema kupatikana kwa dawa mpya ya bedaquiline ni hatua kubwa katika harakati ya kutafuta tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu. Hata hivyo, The Union haikushiriki katika majaribio hao.

Lakini je, kupatikana kwa dawa hii kutasaidiaje katika vita dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ama TB barani Afrika?

Mkurugenzi wa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini Kenya, Dk. Kamene Kimenye, anasema dawa ya bedaquiline imekuwa ikitumika kwa karibu miaka mitatu sasa.

Pamoja na kuwa ni dawa mpya ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu kikamilifu kwa sababu vimelea vinavyousababisha havijaizoea.

Dk. Kamene anasema: ”Kenya tumetumia dawa ya bedaquiline kwa wagonjwa 30 na mataifa mengine pia katika Bara la Afrika kama vile Afrika Kusini na Ethiopia zimekuwa zikitumia.”

Wakati wa Mkutano Mkuu wa Viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, mataifa wanachama walipitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kuchagiza hatua dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Azimio hilo linalofahamika kama “Ushirikiano wa kutokomeza TB: Hatua ya dharura ya kimataifa,” linalenga kutafuta hatua ambayo itachangia kutokomezwa kwa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, ambayo pia ni ukomo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Viongozi hao walisema kuwa wametambua changamoto zilizopo ikiwamo ukosefu wa vifaa, dawa sahihi na hata fedha, bila kusahau jinsi ambavyo TB inasababisha umaskini miongoni mwa familia, jamii na taifa.

Kwa mantiki hiyo, viongozi hao wameazimia pamoja na mambo mengine kutenga fedha zaidi za utafiti na kusaka dawa sahihi sambamba na kuhakikisha hakuna mtu yeyote mwenye TB ambaye hatofikiwa na upimaji na matibabu.

Nje ya mkutano huo, viongozi wa dunia waliahidi dola bilioni 13 kwa mwaka kukomesha maradhi hayo, na dola bilioni mbili zilitengwa kwa ajili ya kugharimia utafiti zikiwa zimepanda kutoka kiwango cha sasa cha dola milioni 700.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, anapongeza hatua ya kupitishwa kwa azimio hilo lenye vipengele 53, akisema lina matarajio makubwa lakini mafanikio yake yatafikiwa iwapo jitihada za pamoja zitawekwa kwenye takwimu bora na sayansi, uamuzi sahihi, kuwezesha jamii na hatua za kimkakati na zilizofadhiliwa.

Anataja changamoto mbalimbali ikiwamo usugu wa dawa, akisema kila mwaka wagonjwa 600,000 wanakabiliwa na usugu wa tiba dhidi ya TB.

“Tunahitaji maendeleo ya kisayansi ili kupata mbinu bora zaidi za kukabiliana na TB, sambamba na tishio la ongezeko la usugu wa dawa za kuua vijidudu vya maradhi.”

Guterres anasema UN itaendelea kufuata mwongozo wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, na shirika lake katika kushinikiza usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa serikali na mashirika ya kiraia na wadau wengine ili kupata kasi inayohitajika katika kutokomeza TB duniani.

Kwa upande wake Dk. Ghebreyesus anataja mambo matatu muhimu yanayoweza kusaidia kufikia lengo la kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.

Mambo hayo ni msaada usiochuja  wa wadau wote utakaofanikishwa na ungwaji mkono na viongozi wa ngazi ya juu kabisa;  Uwekezaji hasa katika sayansi na utafiti, dawa mpya, chanjo mpya na mbinu mpya za utambuzi wa TB pamoja na jukumu la kila mtu kumwajibisha mwenzake.

Dk. Ghebreyesus anasema “Ndio maana tunaandaa mfumo wa uwajibikaji ulio mtambuka ukiwa na misingi mikuu minne: Ahadi, hatua, ufuatiliaji na tathmini kuhakikisha kile tunachosema kinaenda sambamba na tunachotenda.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles