25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dar yazizima mapokezi mwili wa Mengi

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAMIA ya watu jana walijitokeza katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kushuhudia gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi.

Gari hilo lilipita kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi katika Hospitali ya Jeshi Lugalo.

Mwili huo uliwasili saa tisa alasiri kwa ndege ya Emirates kisha saa 10:35 jioni msafara ulianza kutoka uwanja wa ndege kuelekea Hospitali ya Lugalo.

Msafara uliokuwa na magari na pikipiki ulipita katika maeneo ya Tazara, Buguruni, Ilala, Kigogo, Magomeni, Kinondoni, Morocco, Barabara ya Bagamoyo, Sayansi, Mwenge hadi katika Hospitali ya Lugalo ulikohifadhiwa mwili huo.

“Umetuacha na shida zetu baba yetu, tutakukumbuka baba,” hayo ni baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa waombolezaji mbalimbali waliokuwa wakikimbia na gari lililobeba mwili huo.

Wengine walionekana wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali kama vile ‘We believe in your slogan, I can, I must, I will. Rest in Peace Dk. Reginald Mengi’, ‘Sisi viziwi umetuacha mkombozi wetu’.

Katika baadhi ya maeneo watu walilazimika kupanda kwenye maghorofa kushuhudia gari lililobeba mwili wa Dk. Mengi huku wengine wakipanda kwenye madaraja ya juu katika maeneo ya Buguruni na Morocco kwenye kituo cha mabasi ya mwendokasi.

Kuna wakati msafara huo ulisimamishwa kutokana na watu kuingia barabarani kutoa heshima zao za mwisho kwa kulishika gari huku wengine wakitaka kulisukuma kwa mikono.

Maeneo ambako msafara huo ulisimamishwa ni Buguruni, Ilala, Kigogo, Magomeni, Kinondoni na Sayansi.

Baadhi ya waombolezaji wakiwamo wanawake na watu wenye ulemavu walishindwa kujizuia na kuangua vilio huku waombolezaji wengine waliokuwa pembezoni mwa barabara wakionekana kupiga picha.

Mmoja wa waombolezaji aliyekuwa amepakiwa kwenye pikipiki, Asia Jumanne, alisema alimfahamu Dk. Mengi wakati alipowaandalia watu wenye ulemavu hafla ya chakula cha pamoja mwaka juzi.

“Mimi nina mtoto mwenye ulemavu wa akili na nilimfahamu Dk. Mengi mwaka juzi tulipokwenda Diamond kwenye chakula. Ametusaidia sana watu wenye ulemavu ndiyo maana leo (jana) nikasema lazima nije nimuage mzee wangu na kesho (leo) nitakwenda tena kumuaga Karimjee,” alisema Asia.

Mbali ya waombolezaji waliojitokeza katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wafanyakazi wa IPP na wadau wa tasnia ya habari ambao walijitokeza uwanja wa ndege walionekana kuwa na nyuso za huzuni huku wengine wakishindwa kujizuia na kuangua vilio.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ndiye aliyeongoza msafara huo akifuatiwa na viongozi wengine wakiwamo Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia na viongozi wengine.

Mwili wa Dk. Mengi utaagwa leo katika Viwanja vya Karimjee kisha utapelekwa nyumbani kwake Kinondoni na kesho utasafirishwa kwenda Machame mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles