24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza Msigwa kuhojiwa kutoweka kada wa Chadema

ARODIA PETER DODOMA Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema Serikali imeanza uchunguzi wa tukio la kutowekwa kwa kada wa Chadema, Yona Nyagali (Mdude Nyagali).

Vilevile ameelekeza polisi kumtafuta Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema)  alisaidie jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo.

Masauni alisema hayo bungeni jana wakati akitoa taarifa za awali baada ya Msigwa kutoa hoja ya dharura kwa mujibu wa Kifungu cha 47 cha Kanuni za Bunge.

Msigwa aliomba kutoa hoja ya dharura bungeni jana kwa kuliomba Bunge kusimamisha shughuli zake na kujadili kile alichokiita kukithiri kwa vitendo vya mauaji, utekaji na kupotea kwa watu huku Serikali ikiwa haitoi majibu.

“Hivi karibuni katika nchi yetu kumekuwa na matukio ya mauaji, utekaji na watu kupotea, ninapozungumza leo (jana) juzi kuna kijana mmoja anaitwa Mdude Nyagali kule Mbozi ametekwa akiwa nyumbani kwake mbele ya  macho ya watu.

“Alipojaribu kupiga kelele wale watu walionyesha silaha wakamkamata wakamuweka kwenye buti ya gari na kuondoka naye.

“Tumekwenda kwenye vituo vya polisi wamesema siyo wao lakini wamekataa kufungua jalada.

“Mheshimiwa mwenyekiti haya matukio ambayo ukiangalia huku nyuma watu wengi ambao tuliwajadili hata kwenye hotuba ya Mambo ya Ndani tulitaka serikali iji-commit yamekuwa yakiendelea…

“ Sasa trend hii imekuwa ikiendelea na wajibu wa polisi na serikali ni kulinda raia na mali zao, ningeomba mheshimiwa mwenyekiti suala hili tulichukue kwa uzito wake kwa sababu watu wanapotea na serikali haitoi majibu, ningeomba kutoa hoja ili jambo hili liweze kujadiliwa,” alisema Msigwa.

Kutokana na hoja ya Msigwa, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alitoa mwongozo wake akisema: “Suala lolote linalohusu uhai wa binadamu na wa Mtanzania ni suala zito sana, hata hivyo haimaanishi kwamba mtu anapotowekwa… hata mimi nina taarifa jimboni kwangu kuna kijana aliondoka nyumbani kwake tangu juzi hajaonekana hadi leo (jana), sasa haiwezekani mtu ameamua kwenda kwa shughuli zake halafu hakurejea, tuwe tuna…

 “Lakini katika hili ambalo umesema (Msigwa) na wananchi wameona na jitihada zikafanyika lakini bado maelezo yake hayajanyooka vizuri.

“Haitakuwa vizuri sisi wabunge kuanzisha mjadala ambao maudhui yake hatuyafahamu sana, .. ni vema serikali ikatoa maelezo, kama wanaweza sasa hivi au waji-comit baadaye watoe maelezo Watanzania wajue kuhusiana na hali hiyo.

Baada ya maelezo hayo ya Chenge, Mnadhimu wa Shughuli za Serikali bungeni ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliomba mwenyekiti kuruhusu Serikali kutoa taarifa ya awali.

“Ninaomba uridhie angalau kwa hatua ya awali wakati mwingine yanapotokea matukio kama hayo na serikali ikakaa kimya sidhani kama tunajitendea haki sisi serikali na wananchi kwa ujumla.

“Hivyo kwa hatua hii ya mwanzo uturuhusu mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aweze kusema kitu kama anacho cha kusema kwa hatua ya awali,” alisema.

Akitoa taarifa ya serikali, Masauni alisema taarifa iliyotolewa na Msigwa bungeni haina usahihi kwa sababu  jeshi la polisi tayari limeshafungua jalada na kuanza kuchunguza suala hilo.

“ Lakini kutokana na hoja hii mahsusi ambayo Mheshimiwa Msigwa ameizungumza, kwanza nataka nimsahihishe, si vizuri kumuita mbunge mwenzio ni muongo.

“Lakini nimsahihishe na usahihi wa taarifa ambazo amezungumza amesema kwamba huyo mtu ametekwa na vile vile polisi wamekataa kufungua jalada kitu ambacho si sahihi.

“Usahihi wa taarifa ni kama ifuatavyo:  “Ni kweli mtu huyu hakuonekana, hivyo ukisema ametekwa maana yake wewe unajua, sasa kwa sababu Mheshimiwa Msigwa amelithibitishia bunge kwamba mtu ametekwa bila shaka yeye ana taarifa, kwa hiyo nilielekeze Jeshi la Polisi wamtafute Mheshimiwa Msigwa aisaidie polisi”.

 Masauni alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi limeshafungua jalada na serikali inalichukulia kwa uzito suala hilo na  tayari imeshaanza uchunguzi.

“Mpaka   hivi sasa tunavyozungumza jeshi la polisi limeshafungua jalada, si kweli kama Mheshimiwa Msigwa alivyosema na uchunguzi umeshaanza na kuonyesha serikali  imelichukulia suala hili uzito na  tumeongeza nguvu kutoka makao makuu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa jambo hili.

“Kama ambavyo tunachukua uzito kwa matukio yoyote ya uhalifu yanayotokea nchini  tutaendela kulichukulia kwa uzito kama serikali na pale ambako tutabaini kwamba tukio hili limetokea kwa njia ya uhalifu basi hatua zitachukuliwa,” alisema.

Masauni pia ametaka wananchi kuacha vyombo vya dola kufanya kazi yake na kuwaonya ambao wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kwa kuichafua serikali huku akisisitiza watu hao watachukuliwa hatua.

Wakati huohuo, Chadema kimedai kusikitishwa na polisi kushindwa kuzungumzia suala hilo tangu kupotea kwa mwanachama wao mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, alisema Mdude alichukuliwa na watu wasiojulikana Mei 4, ofisini kwake Mkoani Songwe, wakati akiwa anaendelea na majukumu yake.

Alisema  baada ya kutokea   tukio hilo, viongozi wa chama hicho Mkoa wa Songwe walikwenda kituo cha polisi kutoa taarifa lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa.

Alisema tukio hilo siyo la kwanza kutokea chini kwa sababu  kumekua na matukio mbalimbali ya kupotea  wananchi wakiwamo wanachama wao, lakini majibu yanayotolewa na polisi hayaridhishi, jambo ambalo limesababisha kujitokeza shaka.

Alisema kutokana na hali hiyo, chama hicho kitafanya kikao maalumu  baada ya viongozi wao kumaliza ziara za mikoani na kutoa tamko la pamoja na hatua zitakazochukuliwa.

“Kwa sasa viongozi wapo mikoani kwenye shughuli mbalimbali za chama, wakimaliza, watarudi na kuitisha kikao ambacho kitatoa uamuzi kuhusiana tukio hilo pamoja na matukio mengine ya kupotea kwa wananchi yanayojitokeza nchini,hali ambayo inahatarisha amani,”alisema Mrema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles