* Hukata vidole wanawake wanapofiwa na waume zao
Na JOSEPH HIZA,
MILA na desturi za ajabu duniani bado zingalipo pamoja na kuwa kadiri ya miaka inavyosonga mbele na kukua kwa maendeleo na ustawi wa mwanadamu zimekuwa zikitoweka.
Miongoni mwa jamii ambazo bado zina mila za ajabu ikiwamo zilizopitwa na wakati ni pamoja na kabila la Dani linalopatikana huko Papua, Indonesia.
Hivi karibuni wakati wa tamasha la kila mwaka linaloshirikisha kabila hilo na mengineyo jirani yaliyopo katika Bonde Belium kisiwani humo, anaonekana Chifu Eli Mabel wa kabila hilo.
Mkononi anaonekana ameshikilia mabaki ya mmoja wa mababu zake za kale, Agat Mamete Mabel.
Hapo ni katika kijiji cha Wogi huko Wamena, West Papua, kisiwa kilichopo katikati ya Papua New Guinea.
Kabila hilo linaloishi porini katika nyanda za juu za kati za Papua, lina kawaida ya kuhifadhi miili ya mababu zao kwa kuikausha kwa namna ambayo huweza kukaa hivyo kwa mamia ya miaka.
Ukaushaji wa mabaki hayo ya mwili kwa sasa haufanyiki tena, lakini kabila la Dani bado linahifadhi mabaki ya kale lililo kama alama ya heshima kwa mababu zao.
Mbali ya hilo kuna mila ya ukataji wa vidole wasichana na wanawake ikiwa ishara ya kuomboleza kifo cha wapendwa wao wakati wa mazishi.
Mbali ya ukataji vidole kuna upakaji majivu na udongo wa mfinyazi kuonesha huzuni na masikitiko pamoja na marehemu huko aliko.
Kabla ya ukataji vidole, vidole hufungwa kwa uzi kwa dakika 30.
Baada ya kukatwa, kidole kilichokatwa huachwa kikauke kabla ya kuchomwa moto na majivu yake kuzikwa katika eneo maalumu.
Watu wa Dani, ambao huandikwa kama Ndani ni moja ya makabila yenye watu wengi zaidi katika nyanda za juu.
Na wanajulikana zaidi katika Papua kutokana na ziara za mara kwa mara za watalii katika Bonde la Baliem, ambako wanapatikana kwa wingi zaidi.
Kwa mujibu wa Globe na Mail hadi sasa kuna watu 250, 000 wa kabila hilo eneo hilo.
Ukataji vidole ni kitendo kilichotokana na imani ya kidini kwamba iwapo marehemu ni mtu mwenye nguvu wakati akiishi, iwapo hawatafanya hivyo kuna uwezekano wa kutokea maafa.
Kwa sababu hiyo ukataji vidole ni alama ya kuchangia maumivu na marehemu.
Hata hivyo kitendo hicho cha ukataji vidole kinaonesha kupitwa na wakati kwa vile vimepungua vikihusu zaidi kwa sasa wanawake wenye umri mkubwa.
Katika miaka ya hivi karibuni Kabila la Dani limevutia watalii kutoka kote duniani, kwa baadhi ya wanakijiji wakithubutu kuonesha mila zao za asili na kuendesha vita bandia.
Agosti ya kila mwaka kabila hilo hufanya vita hiyo feki na makabila jirani, jamii za Lani na Yali – kusherehekea rutuba na ustawi wa jimbo la Papua pamoja na kufanya ibada za kale za jadi.
Watu wa Bonde la Baliem, makabila ya Dani, Lani na Yali tribes, waligundulika kwa bahati na Mmarekani mtaalamu wa mambo ya kale na mhisani Richard Archbold, wakati akiwa katika safari ya kitafiti nchini New Guinea mwaka 1938.
Katika kabila la Dani, wanaume huvaa mavazi ya jadi, ikiwamo kupaka nyuso rangi, manyoya, mifupa ya wanyama na kibomba cha kusitiri uume kiitwacho Koteka.
Wanawake huvaa siketi zilizotengenezwa kutokana na nyasi, makuto na kadhalika ambazo huvaliwa kuanzia kichwani ikiitwa ‘noken’.