25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kikongwe anayeishi kwa hofu kwa kutuhumiwa mchawi

Marija Marenga akiwa na mdogo wake, Simon Isote.
Marija Marenga akiwa na mdogo wake, Simon Isote.

Na MWANDISHI WETU – RUNGWE

VITENDO vya imani za kishirikina vimekuwa vikijitokeza maeneo mengi nchini na kusababisha mauaji huku wahanga wakubwa wakiwa ni wanawake vikongwe.

Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, zinazoonesha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2014 kulikuwa na matukio ya mauaji ya wazee takribani 1,100 yanayohusishwa na ushirikina katika Kanda hiyo ya Ziwa pekee.

Licha ya kuacha makovu katika familia za vikongwe husika, mauaji hayo yanayotokana na imani za kishirikina yanalifedhehesha Taifa na kulitoa doa kimataifa.

Pia wako vikongwe wengine ambao mali zao zikiwemo nyumba zimeteketezwa, wametengwa katika jamii na kusababisha kuyakimbia makazi yao na kuishi maisha ya hofu.

Katika Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe mkoani Mbeya kumekuwepo na vifo vingi hasa vya watoto katika kipindi cha kilimo ambavyo vinahusishwa na imani za kishirikina.

Wako watu waliowahi kufukuzwa na kutengwa na jamii katika halmashauri hiyo wakituhumiwa kufanya vitendo vya kishirikina baada ya vifo vya utata kutokea.

Tukio la hivi karibuni ni mwendelezo wa matukio mengine mengi yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Hivi karibuni wananchi wa Kijiji cha Bujingijira Kata ya Kandete wilayani humo waliandamana hadi katika ofisi za kata hiyo wakishinikiza kikongwe Marija Malenga (80), kuondoka kijijini hapo kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi.

Kikongwe huyo alifukuzwa jijijini humo siku chache zilizopita akituhumiwa kwa vitendo vya kishirikina ikiwemo kumchanja chale na kiwembe kijana mmoja ambaye hadi sasa anaugua ugonjwa wa ajabu.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa kijiji hicho uliohitisha hivi karibuni, mmoja wa wakazi wa Jonas Kyonya, anadai kuwa bibi huyo amekuwa akikutwa katika nyumba za watu nyakati za usiku akifanya vitendo vya ushirikina.

“Baada ya mkutano huo wanakijiji zaidi ya 700 waliohudhuria, kati yao 300 walitoa maamuzi ya kumtimua bibi huyo na kutoa vyombo vyake nje,” anasema Kyonya.

MTUHUMIWA

Marija Marenga anayetuhumiwa kwa ushirikina, anasema tuhuma hizo si za kweli bali anasingiziwa.

“Sina amani, naishi kwa hofu kubwa kwa sababu kila mtu ananiona mimi mbaya. Niliwahi kuvamiwa usiku nyumbani kwangu na watu wakaniibia fedha nilizokuwa nimetumiwa na watoto wangu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

“Walitoa vyombo vyote nje huku wakitishia kuichoma moto nyumba yangu, nilipoona vile niliamua kukimbilia kijiji cha jirani kwa sababu nilihofia ningeweza kuuawa,” anasema Marija.

NDUGU WA MTUHUMIWA

Mdogo wa bibi huyo, Simon Isote mkazi wa Kijiji cha Ndala, anasema siku ya tukio alikuwa katika shughuli zake za ujenzi na wakati anarejea nyumbani baadhi ya watu walimuita na kumweleza kuhusu tuhuma za dada yake kuhusika na vitendo vya ushirikina kijijini hapo.

“Niliamua kwenda kwa dada yangu na nilipofika nyumbani kwake nilikuta vyombo vyote vipo nje. Nilipomtafuta sikumpata na ndipo nilipoamua kwenda katika ofisi ya kata kuomba msaada,” anasema.

Anasema wakati anaelekea katika ofisi ya kata alikutana na dada yake njiani akitokea kijiji jirani ambako alikuwa amejificha na baada ya hapo waliamua kwenda kwa ofisa mtendaji.

“Tulipofika kwa ofisa mtendaji tulitoa taarifa nay eye alitujibu kuwa anafahamu tukio hilo na akasema kwamba ameuagiza uongozi wa kijiji hushughulikie kwa kuwa yeye alikuwa na ugeni,” anasema.

MWENYEKITI WA KIJIJI

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Edward Mwansule, anasema ni kweli tuhuma hizo dhidi ya bibi huyo zipo.

“Tuliitisha mikutano ya kijiji mitatu na wananchi walimsamehe baada ya kuomba msamaha. Lakini tukio la juzi liliwashangaza wengi ambapo waliamua kumtimua kabisa baada ya kuonekana katika nyumba za watu usiku akifanya vitendo vya kishirikina,” anasema Mwansule.

Anasema baada ya kutokea tukio hilo wananchi walifanya maamuzi magumu ya kuanza kutoa vyombo vyote nje huku wakitishia kuichoma moto nyumba yake.

“Sisi kama serikali ya kijiji tuliamua kuomba msaada kwenye ofisi ya kata ili kusaidia kuwatuliza wananchi,” anasema.

OFISA MTENDAJI WA KATA

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Japhet Boniface, anakiri kuwepo na tukio hilo na kusema kuwa alikwenda kijijini hapo akiwa na askari mgambo wa kata na kukuta vyombo vya bibi huyo vikiwa nje.

“Niliamua kuwakamata baadhi ya viongozi wa kijiji akiwemo Gilbat Mwasunga ambaye ni balozi na kuwatupa lupango,” anasema Boniface.

Anasema baada ya viongozi hao kuwekwa ndani katika ofisi ya kata ndipo kundi la watu zaidi ya 300 walipoandamana ofisini kwake wakitaka watu hao waachiwe huru na kikongwe asirejeshwe kijijini.

Ofisa huyo anasema alilazimika kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu madhara ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni hatari hasa pale ambapo hawana ushahidi wa jambo wanalolidai.

“Kibaya zaidi niliwaeleza Serikali ya Tanzania haiamini uchawi hivyo wanaweza kupata kesi kubwa,” anasema.

Anasema watu hao waliomba msamaha na akaamua kuwaachia huru kwa kuwapa masharti kuwa endapo bibi huyo atadhurika wao ndiyo watakuwa wa kwanza kushughulikiwa.

Ili amani na utulivu urejee na watu waachane na imani za kishirikina katika halmashauri hiyo iliyomegwa kutoka wilayani Rungwe, serikali inatakiwa itoe elimu ya kutosha kwa wakazi wa eneo hilo vinginevyo hali itazidi kuwa tete.

Marija anawakilisha wazee wengine nchini ambao wanakumbana na changamoto kama zake, hivyo ni muda muafaka sasa kupambana kulinda haki za wazee nchini kwani kila mmoja ni mzee mtarajiwa na hakuna ambaye yuko tayari kuishi maisha ya taabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles