26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI: PEMPASI, NEPI INAWEZA KUMSABABISHIA MTOTO KUUGUA FIGO

Dk. Gudila Valentine

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MIAKA ya nyuma watoto wadogo walikuwa wakihifadhiwa kwa kutumia nepi na chupi ya mkojo ili asijichafue au kumchafua mtu anayembeba pindi anapojisaidia.

Lakini kadri siku zinavyosonga mbele kumekuwa na mabadiliko makubwa, leo hii watoto wanahifadhiwa kwa kutumia nepi za kutupa (pampers).

Kwa kawaida pampers hutofautiana bei kulingana na ukubwa, aina na kiwanda ilikotengenezwa lakini huwa ni kati ya Sh 5,000 na zaidi.

Frolence Mussa (si jina lake halisi), mkazi wa Mbezi ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja.

Anasema huwa anatumia nepi na wakati mwingine pampasi, kwa ajili ya kumsitiri mtoto wake lakini huwa inategemea na sehemu alipo.

Anasema; “nikiwa nyumbani huwa namvalisha nepi na mara nyingi huwa ni wakati wa usiku pindi tunapokwenda kulala, lakini tunapotoka kwenda safari au kanisani huwa namvalisha pampasi,” anasema.

Florence anasema mchana huwa hamvalishi nepi wala pampers badala yake humvalisha kampura pekee na kumbadilisha kila anapojisaidia.

“Sipendi kumvalisha nepi wala pampers mchana kwa sababu wakati mwingine huwa zinamchubua, hasa pampasi,” anasema.

“Huwa namuacha anakaa nayo hata saa sita, si anakuwa amejisaidia haja ndogo tu lakini inapotokea amejisaidia haja kubwa inabidi nimbadilishe.

“Napenda kutumia pampasi zaidi tukiwa safari maana anakaa nayo muda mrefu kunakuwa hakuna ule usumbufu wa kumbadilisha kila mara, si kama nepi ambayo unalazimika kumbadilisha mara kwa mara,” anasema.

Shija Mabula ambaye ni baba wa mtoto mmoja anasema huwa anapenda zaidi mtoto wake avae pampasi kuliko nepi.

“Pampasi anakaa nayo muda mrefu hata zaidi ya saa mbili ikiwa hajajisaidia haja ndogo mara nyingi. Huwa tunamvalisha zaidi usiku na tunapokuwa safari,” anasema.

Athari kiafya

Shija na Florence wote hawajui iwapo hatua yao hiyo inaweza kuwasababishia matatizo watoto wao wapendwa katika maisha yao siku zijazo.

MTANZANIA limefanya mahojiano na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Gudila Valentine na hapa anaeleza athari anazoweza kuzipata mtoto kutokana na hatua hiyo.

“Ni hatari kumuacha mtoto muda mrefu akiwa amevaa pampers moja kwani inaweza kumsababishia kupata magonjwa ya UTI na baadae pia anaweza kupata ugonjwa sugu wa figo,” anasema.

Inakuwaje?

Dk. Gudila ambaye kwa sasa anasomea udktari bingwa wa magonjwa ya figo katika Chuo Kikuu Kishirikishi cha Sayansi ya Tiba (Muhas) anafafanua;

“Mtoto akikaa na pampasi au nepi kwa muda mrefu ni hatari kwani husababisha mtoto kupata maambukizi, iwapo anakuwa amejisaidia muda mrefu na kukaa na pampasi au nepi yake, kile kinyesi kinakuwa kama kinarudi, kuelekea kwenye njia ya mkojo.

“Bakteria anayesababisha UTI anaishi kwenye sehemu ya haja kubwa, kwa hiyo lazima mtoto naye asafishwe mara kwa mara kama ilivyo kwa watu wazima ili kumkinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu,” anasema.

Anasisitiza; “lazima usafi uwe kitu cha kwanza. Kwa kuwa bakteria yupo kwenye kinyesi, kinapokaa pale kwa muda mrefu hasa akiwa ni mtoto wa kike kinapata nafasi ya kupanda na kurudi kwenye njia ya mkojo kwa sababu zile njia zimekaa karibu karibu, hivyo inakuwa rahisi kwa yeye kupata UTI.

Anasema ndiyo maana huwa inashauriwa wasafishwe na kubadilishwa nepi au pampasi mara kwa mara kwamba usafi ni suala la msingi na wale watoto wakubwa wasafishwe kutoka mbele kwenda nyuma.

Sababu nyinginezo

Anasema wapo watu ambao hudhani kuwa watoto huwa haugui magonjwa ya figo jambo ambalo si kweli.

“Watoto nao wanaugua magonjwa ya figo kama ilivyo kwa watu wazima, mara nyingi visababishi kwa watoto ni pamoja na hayo magonjwa ya maambukizi kwa mfano ya kuziba kwa njia ya mkojo (UTI) ya kujirudia rudia na kuharisha ambako hutokana na homa ya virusi,” anasema.

Daktari huyo anasema sababu nyingine ni kutapika ambapo husababisha mwili wa mtoto kupoteza maji mengi na kusababisha magonjwa ya figo baadaye.

“Kuna magonjwa mengine kama maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), homa ya ini na malaria sugu, yote haya yanaweza kusababisha mtoto kupata magonjwa ya figo,” anasema.

Dk. Gudila anasema mtoto mwenye lishe duni naye huwa kwenye hatari ya kupata tatizo la figo.

“Mtoto akiwa na lishe duni hupata utapiamlo ambao huchochea baadae kupata magonjwa ya figo, matumizi mabaya ya dawa za kutuliza maumivu jamii ya diclofenac na dawa za kienyeji ambazo huwa zinatokewa bila kiwango maalumu, zote hizi zinaweza kusababisha mtoto kupata magonjwa ya figo,” anasema.

Anasema kuna baadhi ya magonjwa ya kuzaliwa nayo kama kuziba njia ya mkojo na mengine mtoto hurithi kutoka kwa wazazi wake ambayo yanaweza kumsababishia magonjwa ya figo maishani mwake.

Utajuaje njia ya mkojo imeziba?

Dk. Gudila anasema kitu ambacho mzazi ataweza kukiona mapema ni kwamba atakuta mtoto hapati mkojo vizuri mara tu baada ya kuzaliwa, au akikojoa unakuwa na damu.

“Mzazi anapoona mkojo wa mtoto wake unatoka kwa kusita sita au kiwango cha mkojo wa mwanawe kinapungua amuwahishe mapema ili afanyiwe uchunguzi.

“Inapokuwa hivyo ajue tayari kuna shida, au mkojo ukitoka vitone vitone ni tatizo, kawaida mtoto akikojoa mkojo ule unatakiwa uruke mbali lakini si kutoka kidogo,”anasema.

Anasema mtoto anapokuwa amezaliwa ndani ya saa 24 mama anatakiwa awe ameona mwanawe ameanza kujisaidia haja ndogo.

“Sasa unakuta mtoto kakaa hata siku tatu hajakojoa mama hashtuki kama ni tatizo anaendelea kukaa naye nyumbani baadaye sasa ndipo anaanza kuvimba mwili,” anasema.

Magonjwa mengineyo

Daktari huyo anasema magonjwa ya saratani nayo huweza kusababisha mtoto kupata magonjwa ya figo.

“Mtu mwenye saratani ya mfuko wa mkojo ambayo kitaalamu tunaiita ‘blader cancer” anaweza pia kuugua magonjwa ya ndani ya figo ambayo mara nyingi shida huwa inatokea pale kwenye chujio la figo,” anasema.

Jinsi ya kumkinga

Anasema jambo la msingi ni kufuata zile kanuni za afya.

“Tunashauri mtoto anyonyeshwe miezi sita yote ya kwanza baada ya kuzaliwa bila kupewa chakula kingine, hii itamsaidia kupata lishe bora na ni njia nzuri ya kumkinga na maradhi mbalimbali ikiwamo kuharisha, utapiamlo, maambukizi na mengineyo,” anasema.

Anashauri mama ahudhurie kliniki mara kwa mara ili awweze kupata elimu ya jinsi ya kumkinga mwanawe na magonjwa mbalimbali.

“Kliniki wanapewa chanjo pia ambazo huwakinga na magonjwa mengi, mtoto akiugua mpeleke hospitalini atibiwe na si kununua dawa kiholela,” anasema.

Ushuhuda

Asha Juma anasema kuna changamoto nyingi katika kulea mtoto mwenye tatizo la figo.

“Mwanangu ana miaka miwili sasa, alianza kuvimba macho, nilipomlaza kifudi fudi akiamka macho yake yalikuwa yamevimba,” anasema.

Anasema alimpeleka katika kituo cha afya ambapo hawakugundua tatizo lake wakarudi nyumbani.

“Kadri siku zilivyoenda mbele ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya, ukuaji wake ulikuwa si mzuri, nywele zake hazikuota vizuri, miguu na tumbo lake likaanza kuvimba,” anasimulia.

Asha anasema aliamua kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala ambapo aligundulika kuwa na ugonjwa wa figo.

“Waligundua figo yake ina matundu ambayo yanaruhusu maji kuingia mwilini ndiyo maana anavimba miguu na tumbo,” anasema.

Anasema alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako anatibiwa hadi leo.

“Pengine ingegundulika mapema asingekuwa na hali mbaya maana alikuwa akipata malaria mara kwa mara, homa, mafua, na UTI,” anasema kwa huzuni.

Anaongeza kuwa madaktari walimwambia huenda amerithi kwa sababu kwenye familia ya mume wake wapo ambao wanaugua ugonjwa huo.

Anasema changamoto kubwa anayoipata ni kukaa muda mwingi akimtunza mtoto wake huyo na kushindwa kufanya shughuli zake za kiuchumi.

“Sitakiwi kumpa maji mengi, tatizo kwa kuwa ameanza kutembea wakati mwingine akiyakuta anakunywa mengi inakuwa tatizo,” anasema.

Idadi ya wagonjwa Muhimbili

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya watoto na figo Muhimbili, Jacqueline Shoo anasema wanapokea watoto 30 hadi 40 kila mwezi kwenye kliniki yao wakisumbuliwa na magonjwa hayo.

“Asilimia kubwa ya watoto tunaowaona wanaugua magonjwa sugu ya figo sawa na asilimia 60, kuliko magonjwa ya figo ya mshtuko,” anasema.

Chanzo

Anasema sababu kubwa waliyogundua kuwa chanzo cha ugonjwa huo huwa ni magonjwa ya kuharisha, UTI na malaria sugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles