23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI AONYA WANAOTAKA KUUZA FIGO ZAO

Na VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM


DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Onesmo Kissanga amesema kila mwezi watu wawili hufika hospitalini hapo wakitaka kuuza figo zao kwa wagonjwa.

Amesema hata hivyo suala hilo ni kinyume cha sheria za nchi, haliruhusiwi na  halikubaliki.

Dk. Kissanga alisema hayo jana   alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu awamu ya pili ya upandikizaji figo iliyofanywa na madaktari bingwa wa figo wa Muhimbili kwa kushirikishana na wenzao wa Hospitali ya BLK ya   India.

“Wanajitokeza, wanakuja wanataka kuuza figo zao lakini hilo ni kosa, halikubaliki si tu hapa Tanzania bali duniani kwa ujumla, figo haiuzwi,” alisema Dk. Kissanga.

Kuhusu awamu hiyo ya pili ya upandikizaji figo alisema wamefanikiwa kuwapandikiza wagonjwa wanne.

“Tulikusudia kuwafanyia wagonjwa watano hata hivyo mmoja imebidi tumuache na kumfanyia uchunguzi zaidi kabla ya kumfanyia upasuaji huo,” alisema.

Alisema magonjwa ya figo yanazidi kuwa tishio na kwamba utafiti unaonyesha wengi wanakabiliana nayo.

“Nchini inakadiriwa asilimia 6.8 wanakabiliwa na tatizo hili, watu 800 wapo katika huduma ya uchujaji damu na asilimia 60 wanahitaji huduma ya kupandikiza figo,” alisema.

Alisema utafiti unaonyesha magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu yanachangia kwa kiasi kikubwa watu kupata magonjwa ya figo.

“Lakini kwa hapa nchini inaonyesha watu wengi wanapata magonjwa hayo kutokana na kuugua magonjwa ya maambukizi kwa mfano HIV,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Figo wa Hospitali ya BLK ya  India, Dk. Sunil Prakash alisema ni vema watu kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.

“Figo inayopandikizwa huhitajika kutoka kwa ndugu wa karibu wa mgonjwa na lazima washabihiane na figo hiyo iwe salama kwa mgonjwa husika.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema hatua hiyo ya kuwapandikiza figo wagonjwa wanne imewezesha kuokoa   Sh. milioni 300 ambazo zingetumika kugharamia matibabu hayo ikiwa wangepelekwa nje ya nchi.

“Tumeweka mipango ya muda mfupi na mirefu kuhakikisha tunasaidia wananchi hasa wanaosumbuliwa na magonjwa haya kupata matibabu nchini.

“Katika mipango ya muda mfupi tunakusudia kupandikiza   wagonjwa watano kila mwezi, ambako kwa mwaka tutakuwa tumewafanyia wagonjwa 60.

“Katika mipango ya muda mrefu tunakusudia kujenga jengo jipya ambalo ndani yake tutatenga nafasi ya kuhudumia wagonjwa wa figo pekee,” alisema.

Alisema Novemba, mwaka jana hospitali hiyo ilimfanyia upasuaji   mgonjwa mmoja kwa kushirikishana na BLK.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles