Na SAFINA SARWATT-KILIMANJARO
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemkamata daktari wa Hospitali ya Rufaa, Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, alisema jana katika taarifa yake kwamba daktari huyo, Deogratias Urio, alikamatwa Novemba 15, mwaka huu baada ya taasisi hiyo kupokea malalamiko kutoka kwa ndugu wa mgonjwa.
Kwa mujibu wa Makungu, Urio anadaiwa kupokea rushwa ya 150,000 kutoka kwa ndugu wa mgonjwa aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji hospitalini hapo.
“Tulipokea malalamiko kutoka kwa ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akipigwa danadana kupatiwa huduma ya upasuaji hospitalini hapo.
“Katika tukio hilo, daktari huyo alikamatiwa katika Mji Mdogo wa Himo akiwa kwenye baa maarufu ya Mombasa High Way baada ya kuwekewa mtego na makachero wetu.
“Mgonjwa alikuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika kizazi chake tangu Oktoba mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo katika hospitali hiyo na kugundulika ana uvimbe.
“Pamoja na kubainika ana uvimbe huo, mgonjwa hakuweza kupata tiba haraka baada ya kuelezwa na daktari huyo kwamba hawezi kutibiwa hadi atakapotoa fedha hizo.
“Kwa hiyo tunaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo kabla ya kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.
“Pamoja na hayo, tunawaomba madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Mawezi na kwingineko mkoani hapa wazingatie viapo vyao ili hospitali zetu ziwe mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma,” alisema Makungu.