Na AVELINE KITOMARY, Dar es Salaam
SHINIKIZO la juu la damu (presha ya kupanda) hutokea wakati nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya moyo huwa kubwa kuliko kawaida.
Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili kusukuma damu katika mishipa ya damu.
Kwa kawaida ugonjwa wa presha hauna dalili ili ukidumu kwa muda mrefu bila ya tiba kuna madhara makubwa kiafya.
Wataalamu wa afya wanabainisha aina mbili za presha ambazo ni ya kurithi na inayosababishwa na magonjwa mbalimbali.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, asilimia 95 ya wagonjwa wa presha ya kupanda hawana sababu zinazojulikana kisayansi.
Mara nyingi sababu zinazoainishwa ni historia ya ugonjwa katika familia, uzito mkubwa matumizi ya chumvi nyingi, kutokufanya mazoezi, uvutaji sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na umri mkubwa.
Asilimia kubwa ya watu wanaopata ugonjwa presha ya kupanda huwa wanakuwa katika husumbuliwa na magonjwa mbalimbali kama figo, mishipa ya moyo na mfumo wa homoni.
Katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2020 kati ya wagonjwa 334,774 waliotibiwa, asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la presha ya kupanda.
Idadi hiyo ya wagonjwa inadhihirisha kuwa bado kunauhitaji mkubwa wa elimu kwa jamii kuhusu jinsi ya kuweza kuepuka hatari zinazoweza kusababisha shikizo la damu la juu.
Katika kuadhimisha siku ya presha ya kupanda kila ifikapo Mei 17, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliamua kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo na jinsi ya kuuepuka.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa taasisis hiyo, Dk. Samweli Rweyemamu, anasema wamedhamiria ni kutaka jamii kujua sababu hatarishi zinazoweza kusababisha mtu kupata presha ya kupanda.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ‘risk factor’ zinazosababisha shinikizo la juu la damu pia tumeweza kueleza kuwa kuna aina mbili ambazo ni sababu za kurithi na mazingira.
“Sababu zinazotokana na mazingira zinaweza kuzuilika lakini sababu za kurithi kuzuilika inakuwa vigumu au hata ile ya umri kunzia miaka zaidi 65 nafasi ya kupata presha inakuwa kubwa,” anaeleza Dk. Rweyemamu.
MATUMIZI DAWA NGUVU ZA KIUME HATARI
Kwa mujibu wa Dk. Rweyemamu, moja ya matokeo hasi ya matumizi ya dawa za presha na zile za moyo huweza kusababisha kupungua kwa hamu ya ngono (sexual respond).
Anasema hali hiyo imekuwa ikiwakumba wanaume wengi wanaotumia dawa hizo na amekuwa akipata malalamiko ya mara kwa mara.
“Mtu mwenye presha anao uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya moyo na kulingana na tunavyoendelea kupata wagonjwa inaonekana watu wenye shida ya presha na magonjwa ya moyo kwa ujumla ‘side effect’ ya dawa au hata ugonjwa ni kuwa na uwezo mdogo wa kufanya ngono na inaonekana shida hii ni kubwa kwa sababu wagonjwa tunaowaona wengi hasa wanaume huwa wanalalamikia suala hilo.
“Kutokana na suala hilo kuwa tatizo, watu wanatakiwa kujua jinsi ya kuishi nalo kwa sababu shida imeshajitokeza, ukisema usimeze dawa maana yake utapata madhara makubwa kama kupata kiharusi (stroke), moyo na figo kushindwa kufanya kazi, kwahiyo utakuta madhara ni makubwa zaidi,” anasema Dk. Rweyemamu.
Anawasisitiza watu wanaotumia dawa hizo, kuepuka kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa sababu madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi kwa afya ya mtumiaji.
“Kikubwa tunawasihi watu wasinunue dawa hovyo mitaani, hasa zinazoongeza nguvu za kiume kwa sababu ukizichangaya na dawa za moyo bila ushauri wa daktari kwa sababu zinasababisha madhara makubwa, inaweza kushusha presha ghafla mtu akapoteza maisha, hili ni jambo ambalo watu wanatakiwa wafahamu kwa sababu inaweza kuzidi hata presha yenyewe,” anasema Dk. Rweyemamu.
JE, MAJANI YA CHAI YANASABABISHA PRESHA?
Suala la majani ya chai kusababisha presha ni mtazamo uliopo katika jamii ambao bado haujathibitishwa kitaalamu.
Kwa mujibu wa Dk. Rweyemamu, hakuna ushahidi wa moja kwa moja ila kunadhana kwamba majani ya chai yanaongeza kasi ya mapigo ya moyo.
“Ninachojua ni kuwa majani ya chai yana ‘nicotine’ sina ushahidi wa kutosha wala sijaona utafiti unaoonesha kuwa yanaweza kusababisha presha, ninachoweza kusema ni kwamba katika ‘literature’ mbalimbali kuwa majani ya chai yanasababisha mapigo ya moyo kwenda mbio lakini ni chakula ambacho watu wengi tunakitumia pengine ushahidi unaweza kufanyika kuhusu hilo na kuona kama kunauhisiano,” anaeleza.
Dk. Rweyemamu anataja matumizi ya sigara kuwa yana athari kubwa zaidi katika moyo ikiwamo kusababisha presha.
“Sigara inaharibu mwili mzima kuanzia kwenye ubongo, macho, mapafu na inasababisha mishipa ya moyo kuziba na matibabu yake hugharimu fedha nyingi mfano, mishipa ya damu ikiziba ni gharama kubwa kutibiwa.
“Kuacha matumizi ya sigara sio jambo rahisi nalielewa hilo, watu wanaotaka kuacha wanatakiwa kusaidiwa hasa kupata matibabu ya ‘nicotine therapy’ ambazo ziko kidogo kwenye soko,” anabainisha.
MFUMO BORA WA MAISHA Mfumo bora wa maisha unatajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuepuka magonjwa hasa yasiyo ya kuambukiza.
Dk. Rweyemamu anataja mfumo bora wa maisha kuwa suluhisho namba moja ya kuweza kuepuka presha na magonjwa ya moyo.
Anasema aina ya ulaji wa vyakula na jinsi ya ufanyaji mazoezi au kazi hufanya mwili kuwa katika hali ya kukabili magonjwa au kuepuka kabisa.
“Kuna aina ya vyakula na vinywaji mtu anatakiwa kuviepuka mfano kunywa juisi kila wakati, pipi, vitu vingine vyenye sukari na kupunguza chumvi, hivi ni muhimu kitabibu, kingine ni mtu kupunguza uzito kama ni mkubwa kwa sababu unaweza kutumia dawa za presha lakini kama wewe unakilo 150 hata nikikupa dawa za presha zikaisha zote kurudi kawaida inakuwa ni vigimu.
Anasema ni lazima kuweka uwiano mzuri wa afya ya mwili kutokana na dawa za presha siku zote ambazo mgonjwa ataishi.
“Kwanza, dawa za presha au moyo hazikai mwilini au tumboni, zikishatumika zinatoka kwa njia ya mkojo kwahiyo mgonjwa anatakiwa kutumia dawa kila siku.
“Matumizi ya dawa za presha na moyo yataisha pale ambapo uhai wa mhusika utafika mwisho hapa duniani.
“Wakati mwingine tunachokifanya presha ikishuka tunapunguza dozi au kuondoa baadhi ya dawa ili mgonjwa apate dawa inayoendana na presha yake hivyo, kazi yetu ni kurekebisha tu na sio mgonjwa kuacha kutumia dawa kabisa,” anaeleza Dk. Rweyemamu.
LISHE BORA KWA WAGONJWA WA PRESHA/MOYO
Husna Faraji, ni Ofisa Lishe wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), anasema kuwa katika lishe wanatazama mambo mbalimbali ambayo wanaweza kubaini kama mhusika ana lishe bora.
“Tunachoangali ni mhusika anakula nini? kwa wakati gani na anakula kwa kiasi gani? Kwa sababu kama tunavyoona miongoni mwa sababu hatarishi zinazoweza kuchangia kupata presha ni ulaji usiofaa.
“Tunahitaji jamii ielewe kuwa tunapozungumzia ulaji usiofaa ni kutokuzingatia makundi ya chakula na kiasi cha makundi ya chakula, tunasisitiza aina ya makundi ya chakula iliyopo lakini kingine ni kula kwa kuzingatia uwiano uliosahihi.
“Ulaji wa mboga za majani ni muhimu zaidi kutokana na faida nyingi za kiafya zinazopatikana, lakini tunashauri kiwango cha mafuta na aina ya mafuta yanayotumika katika vyakula.
“Ushauri ni kuwa ni bora watu wakatumia mafuta ya mimea badala ya wanyama, hii ni kwa sababu mafuta yanayotokana na wanyama yana ‘cholesterol’ mbaya zinazohusishwa na matatizo ya moyo kwani huziba mishipa ya damu kwenye moyo hivyo kuongeza nafasi ya kuweza kupata presha ya kupanda,” anafafanua.
Husna anasema matumizi ya vyakula vinayosindikwa viwandani ni hatari moja wapo kwa mtu kupata presha na magonjwa ya moyo.
“Matumizi ya vinywaji kama soda ambazo utayarishaji wake huwa unaviwango vikubwa vya sukari hii husababisha shida katika afya ya moyo, tunashauri watu kupendelea vinywaji yenye virutubisho zaidi kama maziwa, juisi ya matunda, maji safi na salama kuliko kutumia viwanywaji vinavyosindikwa kwa muda mrefu kwa sukari na kemikali,” anasema Husna.
Anasisitiza watu kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wanga kwa sababu huchangia matatizo ya moyo.
“Wanga unaongeza uzito kwa hiyo mlaji anakuwa katika nafasi kubwa ya kupata presha ya juu na matatizo ya moyo, magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa kama kisukari, saratani na mengineyo.
“Lakini pia tunasisitiza ufanyaji wa mazoezi kwasababu mtu anayefanya mazoezi tafiti zinaonesha huwa na uwezo wa kupunguza nafasi ya kupata magonjwa, hivyo nashauri hasa tunapokuwa na uzito uliokithiri tuwe na ratiba ya mazoezi kila siku,” anashauri Husna.
Anashauri watu kuweza kuepuka msongo wa mawazo kwa kutafuta haraka njia ya kuweza kutoka katika hali hiyo.