25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Daftari la NEC lasuasua Njombe

Na Michael Mapollu, Njombe
HATUA ya uandikishwaji wa Daftari ya Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa Elektroniki (BVR) katika Mkoa wa Njombe, jana lilianza katika kata tatu za Mjimwema, Yakobi.
Pamoja na kuanza uandikishaji katika kata hizo, yameibuka malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walidai kuwa kasi ya uandikishaji imekuwa ikisuasua huku mwananchi mmoja akiandikishwa kwa muda mrefu.
Katika vituo vya uandikishaji vilivyopangwa katika Kata ya Mjimwema, mwandishi wa habari alitembelea vituo vya kujiandikisha vya Melinze, Mjimwema, Njoss, Mpechi na Joshoni vikionekana kuwa na msululu mrefu wa wananchi waliopanga kujiandikisha.
Changamoto kubwa katika hatua hiyo ilikuwa ni wakati kituo kimoja cha kuandikisha ambako mtu mmoja alikuwa akiandikishwa kwa dakika 20 jambo ambalo lilizua malalamiko kwa wananchi.
“Nipo hapa kwa muda mrefu katika kituo cha Melinze, nimesimama tangu saa 12 alfajiri nikiwahi labda nitaweza kujiandikisha mapema.
“Lakini nilipomuuliza mtaalam wa kuandikisha ni kwa vipi hatua inachukua muda mrefu, alidai picha ninayopigwa ni lazima iende makao makuu Dar es Salaam halafu ndiyo irudi ili kitambulishe kiweze kuwa tayari,” alisema Maria Sanga.
Robert Mkongwa mkazi wa Mtaa wa Melenzi akiwa amejiandikisha, alisema yeye ameshuhudia hatua hiyo ikicheleweshwa na tatizo la vidole vyake kukataa kutambuliwa kwenye mashine kisha kurudia zaidi ya mara tatu.
“Mimi kilichonikuta ni uzoefu wa kuchukua taarifa zangu uandikaji ulikuwa taratibu, alama za vidole ziligoma nimerudia mara tatu ndiyo zikakubali … nimetumia zaidi ya dakika 20 nikiwa ndani mpaka kukamilika na kupata kitambuliusho,” alisema Mkongwa.
Akizungumza juzi kabla ya hatua ya uandikishaji haijaanza, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Njombe, Hilmar Danda, alisema mashine 250 zimesambazwa kwa ajili ya hatua hiyo huku akiahidi kutatua kwa wakati changamoto zilizojitokeza.
“Tume imejipanga vizuri, zile changamoto zilizojitokeza Makambako hakika tutakuwa tumezitatua, NEC itaondoa kasoro hizo kwa wakati,” alisema Danda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles