25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Da Zitta: Filamu za Bongo zinalipa

  • Soko lipo tatizo ni waongozaji na wasanii

NA FESTO POLEA

MAPRODYUZA wanaochipukia katika tasnia ya filamu wengi wao hawafikii malengo waliyojiwekea kutokana na kukatishwa tamaa na baadhi ya wasanii na maprodyuza wenye majina makubwa ambao wanaogopa changamoto za maprodyuza wapya.

Da Zitta 2 Lakini licha ya maprodyuza na wasanii wenye majina makubwa kuwahadaa wasanii na maprodyuza wanaochipukia katika tasnia hiyo wengi wao si wadadisi na hukata tamaa haraka.

Ndiyo, wanakata tamaa haraka kwa kuwa hawataki kuhakiki kama walichoambiwa kina ukweli ama la, wanaridhika na kuamua kuachana na tasnia hiyo huku wakijawa na manung’uniko lukuki bila kujua kwamba walihadaiwa na wasiopenda changamoto zao.

Wengi wamekuwa wakiendelea na dhana kwamba licha ya matumizi makubwa kufanyika katika uandaaji wa filamu ikiwemo kulipa wasanii, madhari, waongozaji, washika kamera, waandishi wa miswada na wengine wengi pia hutakiwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya uhakiki wa kazi zao kwa vyombo husika vikiwemo Bodi ya Filamu, Chama cha Hatimiliki (Cosota) na stempu kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Katika hali ya kuwaondoa woga wasanii na maprodyuza wanaokuja kwa kasi katika tasnia ya filamu ni kwamba, vyombo hivyo husika havina gharama kubwa kama mnavyoshauriwa vibaya na baadhi ya wasanii hao ninaowaita wanaogopa changamoto zenu na wanatumia udhaifu wenu na woga kuwapunguza katika soko la filamu nchini na wao kuendelea kunufaika na filamu zao.

Prodyuza wa filamu ya ‘Gundu’, Zitta Matembo maarufu kwa jina la Da Zitta ambaye hivi karibuni alifiwa na baba yake mzazi, mzee Fidelis Hokororo Matembo, mwanajeshi mstaafu kikosi cha 511KJ Gongo la Mboto, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, anaeleza namna ambavyo wasanii wanakatishwa tamaa huku akiweka wazi kwamba kazi hiyo inalipa na ina mafanikio makubwa kama itafuatwa kisheria.

Da Zitta anasema wanaokatisha tamaa maprodyuza wanaochipukia ni baadhi ya wasanii wenye majina makubwa kwa kuwa hawapendi changamoto ya ushindani kutoka kwa wasanii wadogo.

“Mtaani kuna waigizaji wenye uwezo mkubwa sana kiuchezaji lakini wanapozalisha filamu zao huwa wanakwenda kuomba misaada ya namna ya kufanya ili filamu zao zitoke lakini kumekuwa na ubabaishaji wa baadhi ya wanaowafuata maana wanawakatisha tamaa kwa kuwaeleza kuwa gharama za kupitishwa filamu zao ni kubwa wakati si kweli.

“Mimi nimetoa filamu nyingi na kila filamu niliyopeleka kukaguliwa bodi ya filamu haikuzidi hata shilingi laki na sabini, pia stempu haziuzwi fedha nyingi kama watu wanavyodanganywa na hata kusajili filamu yako Cosota pia si gharama kama zinavyopotoshwa na hiyo yote inatokana na wasanii na maprodyuza wadogo kutokufuatilia mambo kwa vyombo husika kutokana na uvivu na woga wa kijinga,” anafafanua Da Zitta ambaye hadithi za filamu zake anaziandaa mwenyewe.

Da Zitta anaeleza kwamba, biashara ya filamu inalipa sana kama prodyuza atafuata misingi ya kazi hiyo hawezi kukosa faida kwa kila filamu anayozalisha.

“Mimi nakwambia wanaosema filamu za Bongo hazilipi waongo, mbona hakuna anayeacha kwa hao wasanii wakubwa wanaodai hailipi, kinachotakiwa uandae hadithi nzuri, picha zake ziwe na ubora na pia waigizaji waonyeshe vipaji vyao utauza na faida utapata soko lipo na wadau wa filamu wanataka filamu za wasanii kutoka mtaani kwa kuwa ndiko kwenye vipaji vipya vilivyokosa sehemu ya kujionyesha.

“Wapo wengine wakishamaliza kuandaa filamu wanadhani lazima wazipeleke kwenye soko la Wahindi ambao ndio wauzaji pekee na wanazidiwa na soko,  wanasahau kwamba kuna njia nyingi za kusambaza kazi hizo.

“Mimi niliwahi kupeleka kazi yangu kule lakini baada ya kukaa sana bila kutoka niliifuata wakanipatia lakini baada ya muda niliiona ikiwa imetoka na sikupewa fedha yoyote lakini kwa kuwa nilifuata vyombo vyote husika niliwashtaki nikalipwa ingawa kilikuwa kiasi kidogo na kuanzia hapo niliachana na kupeleka kazi zangu kwa Wahindi nikaamua kuanza kusambaza kwa mawakala wa mikoani kwa oda maalumu,” anaeleza Da Zitta.

Da Zitta anasema kwa kuwa ukisambaza mwenyewe unapata faida kubwa anafanya maandalizi ya kuanza kununua kazi za wasanii wanaochipukia ili kukuza soko lao na kuonyesha mchango wangu kwao.

“Mimi nasisitiza kwamba filamu zinalipa lakini zikifuatwa taratibu maana kama nisingefuata taratibu nilipokuta filamu yangu inauzwa bila mimi kulipwa nisingeweza kudai na kulipwa. Kingine wasanii na maprodyuza wanatakiwa kujitambua na kujiongeza kwa  kuomba ushauri kwa vyombo husika ili wasiweze kudanganywa kuhusiana na elimu ya filamu na mafanikio yake,” anamaliza Da Zitta ambaye licha ya filamu ameingia katika muziki na amesharekodi wimbo na rapa, Mr Blue.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles