Na KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
BODI ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imemfungulia kesi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Katika shauri hilo, bodi hiyo inaiomba Mahakama Kuu ya Tanzania itoe amri ya kumzuia msajili asifanye kazi nje ya mamlaka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika mahakama hiyo, Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya msajili huyo, Profesa Ibrahimu Lipumba na wanachama 12 waliofukuzwa katika chama hicho.
Akizungumza baada ya kuwasilisha kesi hiyo mpya masijala kuu, Wakili wa Wadai, Juma Nassoro, alidai shauri limefunguliwa baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa msajili huyo wa vyama vya siasa.
“Tunaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia msajili kufanya kazi nje ya mamlaka aliyonayo kwa sababu Mahakama Kuu ilishawahi kutoa hukumu ikisema msajili hana mamlaka ya kuingilia mambo yanayoendelea ndani ya vyama vya siasa.
“Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya vyama ni kuharibu demokrasia,”alidai Nassoro.
Nassoro alisema kesi imekwisha kufunguliwa na sasa kinachosubiriwa ni taratibu za mahakama kwa ajili ya kuipa namba.
Hivi karibuni, Jaji Mutungi alitoa hoja 11 zilizomrejesha Profesa Lipumba katika wadhifa wake wa Mwenyekiti wa CUF.
Mbali na Profesa Lipumba, viongozi wengine ambao msimamo wa Msajili uliwarejesha madarakani moja kwa moja baada ya kusimamishwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililokaa Agosti 30, mwaka huu Dar es Salaam, ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.
Wengine ni Naibu Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya, Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma, wajumbe wa Baraza Kuu, Masudi Omari Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa na Kapasha Kapasha.
Katika barua yake kwa viongozi wa CUF, msajili alisema alitoa msimamo huo baada ya kusikiliza pande zote zinazopingana katika mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema alifikia uamuzi huo kwa kuzingatia mamlaka na wajibu wa msajili kushughulikia mgogoro huo na kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
Pia, alisema alizingatia Profesa Lipumba kutengua barua yake ya kujiuzulu, uhalali wa mkutano mkuu maalumu wa CUF wa Agosti 21, mwaka huu na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu maalumu kuhitaji Profesa Lipumba aitwe katika chumba cha mkutano kujieleza.
Sababu nyingine ni uhalali wa kura zilizopigwa kukubali au kukataa Profesa Lipumba kujiuzulu, uhalali wa kikao cha baraza kuu la uongozi Agosti 28, mwaka huu na utaratibu wa kuchukua hatua za nidhamu.
Nyingine ni uhalali wa kamati iliyoundwa na baraza kuu la uongozi la Agosti 28 ili kufanya kazi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na uhalali wa uteuzi wa viongozi wa taifa uliofanywa na kikao cha baraza kuu la uongozi Agosti 28, mwaka huu.
Kesi hiyo imefunguliwa huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa katika CUF, upande mmoja ukiwa unamuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalum Seif Sharif Hamad na mwingine wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.
Mgawanyiko huo ni wa wanachama, viongozi hadi Bodi ya Wadhamini.
Siku chache zilizopita wajumbe watatu wa Bodi ya Wadhamini wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Abdallah Katau, walikutana Zanzibar na kutangaza kutomtambua Profesa Lipumba ikiwamo kumfukuza uanachama wa chama hicho.
Juzi wajumbe ‘watano’ wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho walikutana Dar es Salaam na kusema kuwa tamko la wajumbe wa bodi hiyo waliokutana Zanzibar ni batili na hivyo Profesa Lipumba anaendelea kutambulika kama mwenyekiti wa chama hicho.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Peter Malebo, alisema wao hawatambui tamko lililotolewa na mwenyekiti wao ikizingatiwa bado inajiandaa kuwakutanisha Profesa Lipumba na Maalim Seif kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Bodi ya Wadhamini ya CUF inaundwa na wajumbe wanane, watano kutoka Bara na watatu kutoka Zanzibar.
Wajumbe hao ni Abdalah Katau, Peter Malebo, Ally Mbarouk, Amin Mrisha, Zacharia Kwangu, Yohana Mbelwa na Dk. Juma Muchi.