28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yalia uandikishaji mdogo Zanzibar

CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF),  kimesema kimesikitishwa na  vikwazo vya uandikishwaji mdogo  wa wapiga kura Zanzibar kwakuwa vinaweza kuchangia kuwanyima haki wapiga kura wakati wa  uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa  Ibrahim Lipumba alisema kimsingi Tume ya Uchaguzi Zanzibat (ZEC), inaandikisha daftari jipya la wapiga kura ambao wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya ukaazi –Zan – Id Mpya, lakini wengi hawajapewa.

Alisema ukosefu wa vitambulisho vya Zan- Id, itachangia kuwanyima fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao na kusababisha uiingie dosari kwa kuwa utakuwa si huru na haki.

“Kwa mfano idadi ya walioandikishwa Jimbo la Konde, ni 4,331, ukilinganisha na wapiga kura 9,299 walioandikishwa uchaguzi wa mwaka 2015, Jimbo la Wete mwaka 2015 walioandikishwa walikuwa 8,574,mwaka huu hadi sasa wameandikishwa 3,597,”alisema Lipumba.

Alisema wananchi wengi wenye sifa ya kuandikishwa kuwa wapiga kura, wamenyima fursa hiyo, baada ya kunyimwa vitambulisho.

“Tunaweza kuamini sababu za kisiasa zimechangia watu hawa kunyimwa vitambulisho, Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere alieleza haki ndiyo msingi wa amani, Wazanzibar wana haki ya kupiga kura na kuchagua wawakilishi wanaowataka,” alisema.

Alisema  Baraza Kuu la Uongozi  la chama hicho, limeitaka ZEC kuwaandikisha wananchi wenye sifa bila kujali ubaguzi ili kuwa na orodha ya wapiga kura ambao ni halali.

Pia limeagiza Kamati Tendaji ya Taifa kuharakisha mchakato wa kutoa kalenda ya mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wanachama watia nia wa nafasi mbalimbali kwa Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema mbali ya mazingira mabaya ya kisiasa yaliyopo hivi sasa, chama hicho kitasimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Katika hatua nyingine, aliiomba Serikali kushirikiana na jumuiya za kimataifa, hasa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuandaa mkakati madhubuti wa kukabiliana na mlipuko wa  virusi vya COVID-19.

Alisema tayari Benki ya Dunia , Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), imetangaza kuwapo kwa mifuko ya dharura ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles