CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kitaendelea kusimamia na kulinda chaguo la wananchi katika Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Pamoja na hali hiyo, CUF imesema bado inatoa nafasi kwa Rais Dk. John Magufuli kutokana na jitihada anazozifanya katika kuupatia ufumbuzi wa haraka mgogoro wa Uchaguzi wa Zanzibar ambao matokeo yake yamefutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema pamoja na kile alichokiita hila, amewataka wananchi kupuuza taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Jussa alisema taarifa ya Waride ni sawa na kufunika kombe kutokana na maswali wanayoulizwa na wanachama wao juu ya kutumia mabilioni ya fedha, lakini wakashindwa vibaya kwenye uchaguzi.
“Taarifa ya CCM Zanzibar iliyotolewa na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi inaonyesha jinsi chama hicho kisivyojali madhila wanayoyapata raia, fedheha iliyopata taifa na hali ya kiuchumi inayozidi kudorora kila siku Zanzibar ikiwaathiri mno wananchi wanyonge.
“Taarifa inazungumzia uchaguzi wa marudio, lakini papo hapo Katibu wa Uenezi CCM Zanzibar anasema CCM haina imani na Tume ya Uchaguzi iliyopo na kwa hivyo uchaguzi huo wa marudio lazima ufanyike chini ya tume mpya.
“Baada ya hapo hasemi tume iliyopo ambayo muda wa utumishi wa makamishna wake unalindwa kikatiba itaondolewa vipi na tume mpya itapatikana vipi,” alisema Jussa.
Jussa ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliwahakikishia Wazanzibari kuwa CUF kama chaguo lao haitotetereka na kusimamia kwa dhati uamuzi wao walioufanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu.
Kutokana na hali hiyo, Jussa aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kuonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya Oktoba 25, mwaka huu.
Oktoba 28, mwaka huu, Jecha alitangaza kufuta uchaguzi huo mbele ya waandishi wa habari mjini Unguja akisema haukuwa huru na wa haki, baada ya kukabiliwa na vikwazo vingi katika kutekeleza majukumu yake.
Jecha alitaja vikwazo tisa alivyokabiliana navyo ambavyo alidai vimechangia ZEC kuchelewesha matokeo ndani ya muda uliopangwa kisheria.
Alisema kutokana na hali hiyo kulibuka mizozo na kutoelewana kwa makamishna wa ZEC hali iliyofikia wengine kuvua mashati na kutaka kupigana.
Jecha alisema ni dhahiri baadhi ya wajumbe badala ya kuwa makamishna wa tume wakageuka kuwa ni wawakilishi wa vyama vyao vya siasa.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema hakubaliani na uamuzi huo na kudai kuwa kuna njama zinazofanywa na si kweli kama uchaguzi huo haukuwa wa haki.
“Tunatamka wazi kwamba CUF hatuutambui uamuzi huo binafsi wa Mwenyekiti wa Tume na tunaitaka Serikali na CCM kuiacha tume iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi,” alisema Maalim Seif.
Alisema CUF imeonekana wazi kwamba ni mshindi wa uchaguzi wa Rais pamoja na majimbo yote 18 ya Pemba na majimbo mengine tisa ya Unguja.
SHEIN NA MAGUFULI
Desemba 24, mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, Ikulu, Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo ya mwenendo wa kisiasa visiwani humo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni Dk. Shein kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu hali ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa wa Zanzibar.
Ilieleza kuwa Rais Shein alisema mazungumzo yanaendelea chini ya Kamati Maalumu ya kutafuta suluhu iliyo chini ya uenyekiti wake.
Kamati hiyo inaundwa na Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Pia wamo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Salmin Amour.