Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
VIONGOZI wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Bahi, wametoa tamko la kupinga Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba na kusema kuwa si kiongozi halali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Katibu wa CUF Wilaya ya Bahi, Omari Makomba, alisema wao wataendelea kuheshimu taratibu za chama kwa kumtambua Julius Mtatiro kama Mwenyekiti halali wa Kamati ya Uongozi.
“Profesa tunaona na kusikia yupo katika baadhi ya maeneo akifanya ziara. Sisi kwetu Bahi tunasema kabisa kama akija hatutampa ushirikiano wa aina yoyote.
“Tunayemtambua ni Julius Mtatiro, ambaye ni kiongozi halali. Ila kwa Lipumba hicho anachokifanya ni matakwa yake binafsi, nasi kama wana CUF katika kikao chetu cha Kamati ya Utendaji tumeazimia kutomtambua na wala hatuwezi kumpa ushirikiano,” alisema.
Mgogoro wa CUF hivi sasa umefikishwa Mahakama Kuu ukisubiri uamuzi ambapo baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wamemshtaki Msajili pamoja na Profesa Lipumba na wenzake kwa kuvunja taratibu za chama, licha ya kuvuliwa uanachama kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.