27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Vyama vya siasa vifuate sheria ili visifutwe

francis-mutungi

ALHAMISI wiki hii kuliripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa Chama cha APPT-Maendeleo kinachoongozwa na Peter Mziray, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, ni miongoni mwa vyama vitatu vilivyofutwa kwenye daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kwamba kutokana na hali hiyo, Mziray anapoteza sifa ya kuongoza Baraza hilo ambalo lipo kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kwamba hatua ya kukifutia usajili chama hicho inatokana na kufungua duka la kuuza vyombo vya muziki kwenye ofisi kuu yake kuu iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam.

Akizungumza ofisini kwake Jumatano wiki hii, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alivitaja vyama vingine vilivyofutiwa usajili kuwa ni Chama cha Haki na Ustawi (Chausta) kilichosajiliwa Novemba 15, 2000, kilichokuwa kinaongozwa na James Mapalala na Katibu Mkuu wake, Mwaka Mgimwa.

APPT-Maendeleo kilipata usajili Machi 4, 2003 na kilikuwa kinaongozwa na Mziray na Katibu Mkuu, Nziamwe Samwel.

Jaji Mutungi alitaja chama kingine kilichofutiwa usajili kuwa ni Jahazi Asilia, kilichosajiliwa Novemba 17, 2004. Mwenyekiti wake ni Kassim Ally na Katibu Mkuu, Mtumweni Seif.

Hatua hiyo inatokana na upungufu wa jumla uliobainika kuwamo ndani ya vyama hivyo; yaani kutokuwa na ofisi Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu namba 10 (d) cha Sheria ya Vyama vya Siasa; kutokuwa na wanachama Zanzibar kwa mujibu wa kifungu 10(b) na kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi kwa mujibu wa kifungu 14(1)(a).

Kwamba kushindwa kuwasilisha hesabu zao za mapato na matumizi ya mwaka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kushindwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tamko la orodha ya mali za chama na kushindwa kutekeleza matakwa ya kifungu cha 15(1) kwamba mapato yote ya fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama ni makosa na kinyume cha utaratibu wa vyama unavyopaswa kutekelezwa.

Mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivi unatokana na uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia Juni 26 mpaka Julai 26, mwaka huu.

Kwamba APPT-Maendeleo kimekutwa na jumla ya makosa sita, likiwamo la kutokuwa na ofisi Bara, baada ya kugeuza ofisi yake kuwa duka la vifaa vya muziki, wakati ile ya Zanzibar ikiwa ni chuo cha kompyuta.

Tunasema madai ya Mziray  kuwa Msajili ana chuki binafsi bila kufafanua chuki hizo; na kukiri kuwa ofisi ya makao makuu ya chama hicho imegeuzwa duka la vifaa vya muziki ni kukosa hoja za utetezi na kukubali makosa.

Tunadhani kuendesha chama cha siasa kuna utaratibu wake ambao unapaswa kufuatwa.

Tunasema masharti ya kuandikishwa kuwa chama cha siasa na uendeshaji wake yanahitaji utekelezwaji wa masharti yaliyotajwa hapo juu.

Tunasisitiza kuwa, vyama vyote vya siasa havina budi kujua masharti haya ili visikumbane na mkono wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles