HAVANA, CUBA
WACUBA wameanza kipindi cha siku tisa za maombolezi ya aliyekuwa rais wao na kiongozi wa mapinduzi nchini hapa, Fidel Castro.
Mdogo wake, ambaye ndiye aliyemrithi urais, Raul amesema mwili wa kaka yake aliyefariki juzi utachomwa moto kwa utashi wa kiongozi huyo.
Majivu ya Castro yatazikwa katika mji wa Santiago de Cuba baada ya siku nane za maombolezi ya kitaifa yatakayohitimishwa Desemba Nne.
Umma utaruhusiwa kushuhudia mwili wa Castro leo na kesho katika eneo la makumbusho la Jose Marti mjini Havana kabla ya kufanyika sala maalumu ya kumuaga kwenye uwanja mkuu wa mapinduzi mjini hapa.
Gwaride la nchi nzima litafuatia katika muda wa siku nne, kwa matembezi ya kilometa 900, na mkutano mkubwa wa pili wa sala maalumu utafanyika Jumamosi.
Maafisa wa Cuba wamesema tukio la mazishi linatarajiwa kufanyika katika makaburi ya Santa Ifigenia mjini Santiago, Desemba Nne.
Katika kipindi cha maombolezi hakutakuwa na shughuli au matamasha ya wazi, bendera zitapepea nusu mlingoti katika majengo ya serikali huku radio na televisheni zikitarajia kutangaza vipindi vya taarifa, uzalendo na historia, maafisa wamesema.
Picha za hivi karibuni zilizochapishwa za Fidel Castro zilitoka  Novemba 15 mwaka huu wakati alipokutana na Rais wa Vietnam, Tran Dai Quang.
Na tukio lake la mwisho kuonekana hadharani lilikuwa Agosti 13 katika ukumbi wa matamasha wa Karl Max mjini hapa.
Tangu alipoondoka madarakani mwaka 2006, Fidel Castro alijing’atua kutoka katika siasa.
Afya ya Castro iliwekwa siri kwa kiasi kikubwa nchini Cuba na hadi sasa hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu sababu za kifo chake.