Eliya Mbonea, Arusha
Benki ya CRDB imeahidi kuwasimamia vizuri wajasiriamali wadogo (Machinga) waliopewa vitambulisho na serikali ili wainuke kimtaji.
Kauli hiyo imetolewa mjini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, katika semina iliyotolewa na benki hiyo kwa wajasiriamali.
“Hii ni fursa kuwatambua wajasiriamali waliopewa vitambulisho, tutawasimamia ili tuwainue kimtaji, Serikali ikimwamini mtu CRDB ni nani tusimwamini na kumhudumia,” amesema Nsekela.
Kwa upande Gambo amewashukuru wafanyabiashara walioshiriki semina hiyo iliyolenga kuwafundisha masuala ya huduma za kifedha zitolewazo na benki hiyo.
“Napongeza juhudi hizi, hili ni kundi muhimu katika kutimiza adhma ya Rais Dk. John Magufuli ya kujenga Tanzania yenye uchumi wa kati wenye kutegemea viwanda, yaani “Tanzania ya viwanda,” amesema Gambo.