28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB yajivunia mikopo kwenye kilimo, yamtaja Rais Samia

Na Clara Matimo, Mwanza

WAKATI Tanzania ikipambana kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 kutoka asilimia tano ya sasa ifikapo mwaka 2030, Benki ya CRDB imejivunia kutoa mchango chanya kwenye sekta hiyo katika miaka miwili iliyopita kwa kutoa mikopo kwa wakulima.

Katika kuadhimisha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, benki hiyo inajivunia kutoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh Trilioni 1.6 katika sekta ya kilimo nchini kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa awamu ya sita.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima akizungumza kwenye kongamano hilo.

Hayo yameelezwa na Meneja wa benki hiyo Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta wakati wa kongamano la miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan ambalo limefanyika Machi 15, 2023 katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza.

Sitta alisema hatua hiyo ni baada ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuzitaka taasisi za fedha nchini kushusha riba kwenye mikopo ya kilimo na ufugaji na kuwa chini ya asilimia 10, ambapo CRDB katika kuitikia wito huo imeshusha riba hiyo kutoka asilimia 16 hadi 20 ya awali mpaka asilimia 9 ya sasa.

“Benki ya CRDB kwa mwaka jana tumetoa mikopo inayofikia Sh bilioni 801 hii ni asilimia 43 ya mikopo yote nchi nzima, kwa upande wa mikoa ya Kanda ya Ziwa tumetoa zaidi ya Sh bilioni 200 yote tunachaji kwa riba ya asilimia tisa maana ni ya kilimo agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuyataka mabenki yaweze kuchagia ukuaji wa uchumi wa wananchi  kwa  kutoa mikopo yenye asilimia ndogo  ya riba umeleta tija sana kwa sababu mikopo hiyo pia inalipika kiurahisi.

“Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameleta mabadiliko makubwa sana kwa ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa kweli amesimamia vizuri sana mazingira ya biashara katika upande wa fedha maana hata upande wa taasissi za fedha kuna matokeo chanya,”alisema Sitta na kuongeza

 “Kabla ya tamko lake wakulima walikuwa sawa na makundi mengine yanayochukua mikopo maana makundi mengine tunatoa mikopo yenye riba ya asilimia 20 hadi 21 aliona benki zikitoa mikopo yenye riba ndogo hata uzalishaji wa bidhaa utaongezeka kwa sababu gharama inakuwa iko chini, hakika benki ya CRDB tunajivunia sana miaka miwili ya uongozi wa Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”alisema Sitta.

Baadhi ya watu kutoka makundi mbalimbali waliohudhuria kongamano la miaka miwili ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani lililofanyika Machi 15, 2023 katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati mkoani humo ikiwemo ujenzi wa  daraja la Kigongo- Busisi  na meli ya Mv Mwanza Hapa  Kazi tu kwa kuendelea kutoa fedha za wakandarasi.

“Mbali na miradi mikubwa ya kimkakati pia serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa Mkoani Mwanza, lengo la Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuboresha viwango vya maisha vya kila Mtanzania,”alisema Malima.

Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu isemayo ‘Hakuna kilichosimama Mkoa wa Mwanza lilihudhuriwa na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi binafsi, viongozi wa dini na wananchi ambapo kila kundi lilielezea jinsi lilivyonufaika kutokana na utekelezaji wa shughuli za serikali zilizofanywa kwa kipindi cha miaka miwili chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, 2021 kutokana na mtangulizi wake hayati Dk. John Magufuli kufariki Machi 17, 2021.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles