23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TARI yataka Watafiti wa mbegu kuzalisha mbegu zenye ubora

Na Gustafu Haule,Pwani

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI), Dk. Geoffrey Mkamilo, amewataka watafiti wa kilimo nchini kufanya utafiti na kuzalisha mbegu bora kwa wingi ili ziwafikie wakulima na hivyo kuongeza uzalishaji.

Dk. Mkamilo ametoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kituo cha Kibaha kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kiutafiti katika kituo hicho ambacho kina dhamana kitaifa katika kufanya utafiti wa mazao ya miwa,mihogo na viazi vitamu.

Dk. Mkamilo amesema  kipaumbele cha serikali kwa sasa ni uzalishaji wa mbegu bora ambazo zitawafikia wakulima kwa wakati kwani serikali imeongeza fedha karibu maradufu kwenye utafiti lengo likiwa ni kuwaondolea wakulima changamoto wanazokutana nazo katika kilimo.

“Kipaumbele chetu kwa sasa ni kuona wakulima wanapata mbegu bora,nataka kuona TARI Kibaha na vituo vingine vilivyopo maeneo mbalimbali hapa nchini vinafanya utafiti wa mbegu na kuzalisha mbegu bora na zenye tija kwa wakulima,”amesema Dk. Mkamilo.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa katika kuwahudumia wakulima na kuboresha bajeti ya wizara ya kilimo hivyo ni jukumu la watumishi wa taasisi hiyo kutimiza wajibu wao kikamilifu.

“Kila mtumishi lazima atimize majukumu yake kikamilifu,kwa sasa hakuna kisingizio cha kushindwa kufanya utafiti na kuzalisha mbegu bora kwa wakulima kwani serikali imetupa nyenzo zote muhimu za kufanyia kazi ikiwemo  kuwepo kwa mipango thabiti ya kushughulikia stahiki za watumishi,” amesema Dk Mkamilo.

 Hata hivyo, Dk. Mkamilo ametoa wito kwa watafiti kujenga utamaduni wa kuandika maandiko na kutafuta fedha kwa ajili ya kupanua shughuli za utafiti badala ya kutegemea vyanzo vichache vya fedha.

Akielezea namna kituo hicho kinavyofanya kazi Meneja wa TARI Kibaha Dk. Nessie Luambano amesema kuwa kwa sasa idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 32 na kufikia 53 baada ya serikali kuajiri watumishi wapya na wengine kuhamia kituoni hapo kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dk. Luambano, amesema kutokana na kuongezeka kwa watumishi, TARI Kibaha imeendelea kufanya utafiti na kuzalisha mbegu kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya za Kilombero,Kilosa,Mvomero na Misenyi ambapo kwa mwaka huu wa fedha kituo chake kimeanza uzalishaji wa mbegu ambapo jumla ya ekari 55 zitazalishwa.

Amesema, mbegu hizo zikishazalishwa zitasambazwa kwa wakulima ambapo  zoezi kama hilo hufanyika mara kwa mara na limesaidia kuhakikisha wakulima wengi wa miwa nchini kupata mbegu bora na salama zilizosaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari nchini.

“Kwa ujumla mipango yetu ni kuhakikisha kila sehemu ambapo wakulima wanalima miwa ya sukari wanapata mbegu zilizo bora hivyo kama kituo ambacho tuna dhamana katika zao hilo tunafanya kila tunaloweza ili wakulima wapate mbegu bora,” amesema Dk. Luambano.

Dk Luambano amemshukuru Rais Dk Samia kutokana na kuboresha mazingira ya utendaji kazi hasa kwa kuendelea kuajiri wataalam katika sekta ya utafiti na hivyo kupanua wigo wa kituo chake kutekeleza majukumu yake.

Mratibu wa zao la miwa Kitaifa, Minza Masunga,alimweleza Mkurugenzi Mkuu wa TARI kwamba mwaka wa fedha uliopita walizalisha mbegu katika Wilaya ya Kilosa,Kilombero na Mvomero mkoani Morogoro ambapo mbegu hizo zimeanza kupandwa kwa wakulima wa miwa mkoani humo.

Hatahivyo, Minza ameeleza kwamba uwepo wa mashamba darasa katika mkoa wa Morogoro kumeongeza idadi ya wakulima walioamua kuingia katika kilimo hicho huku wataalam wa TARI Kibaha wakishirikiana bega kwa bega na wakulima katika kukabiliana na changamoto za wakulima ikiwemo wadudu na magonjwa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles