27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB yaeleza sababu ya Kimei kung’atuka kabla ya muda

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB imeeleza sababu za kumpumzisha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk. Charles Kimei, kabla ya muda wake kumalizika.

Mkurugenzi Mtendaji mpya, Abdulmajid Nsekela, aliripoti ofisini Oktoba Mosi na Oktoba 2 alikabidhiwa rasmi ofisi na kuanza kazi.

Awali bodi hiyo ilieleza kuwapo kwa kipindi cha mpito cha takribani miezi minane ambacho Nsekela angefanya kazi na Dk. Kimei.

Akizungumza   Dar es Salaam jana wakati wa kumtambulisha Mkurugenzi mpya wa benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Ally Laay, alisema walikutana Oktoba 2 mwaka huu na kupitisha uamuzi kuwa Dk. Kimei apumzike.

“Tuliamua Dk. Kimei apumzike na kumpisha Mkurugenzi Mtendaji mpya kwa kutilia maanani misingi ya utawala bora na maadili yetu ya kazi kuwa ingeleta ugumu kwa benki kuwa na wakurugenzi watendaji wawili kwa pamoja kwa kipindi kirefu,” alisema Laay.

Alisema walijiridhisha kuwa Nsekela ni mtu sahihi na ana weledi, ujuzi, umahiri na uzoefu wa kutosha kuiongoza benki hiyo hivyo kutohitaji kushikwa mkono kwa muda mrefu kama ilivyoamuriwa   awali.

“Kwetu sisi Nsekela ni kijana na askari wetu wa miamvuli anayerejea nyumbani, ni mtu makini na sahihi wa kuiongoza Benki ya CRDB kuingia kwenye zama mpya zinazotilia mkazo mapinduzi ya teknolojia,” alisema.

Bodi hiyo ilisema inatambua mchango wa Dk. Kimei katika kujenga na kubadilisha benki hiyo kuwa chaguo namba moja kwa wateja nchini na kwamba utaandaliwa utaratibu wa kumuaga kwa heshima zote.

Desemba mwaka jana, Dk. Kimei alitangaza kustaafu nafasi yake ndani ya benki hiyo baada ya kuiongoza kwa miaka 20.

Alisema alichukua uamuzi wa kutoongeza mkataba   kwa hiari na kwamba atabaki kuwa mwanahisa na mteja wa benki hiyo.

MKURUGENZI MPYA

Naye Nsekela alisema mabadiliko ya uongozi katika benki hiyo hayataleta tatizo na benki itaendelea kuwa imara na wateja wataendelea kupata huduma bora.

“Naishukuru bodi kwa kujenga imani kubwa kwangu na kuona nastahili kuchukua kijiti cha Dk. Kimei ikizingatiwa   ukubwa wa taasisi hii,” alisema Nsekela.

Alisema amedhamiria kufanya maboresho makubwa katika benki hiyo hasa katika utoaji huduma kwa wateja kwa kutilia mkazo maeneo matano muhimu.

Kwa mujibu wa Nsekela maeneo hayo ni uboreshaji wa mifumo na taratibu za utoaji huduma, kuongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi, kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa, kukuza biashara  kuendana na kasi ya Serikali.

“Biashara ya benki imekua lakini inabidi kukua zaidi, na Benki ya CRDB ni kubwa   na inafanya vizuri kwa muda mrefu lakini ukubwa huu tusipouangalia kwa makini kuna wadogo wanaweza kutushinda,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema benki itajikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya digitali itakayowezesha kuwafikia wateja wengi zaidi na kuwaondolea ulazima wa kutembelea matawi ya benki.

Nsekela ni mtaalamu na mbobezi wa masuala ya biashara ya benki mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika sekta ya benki.

Alianza kazi kama Mshauri wa Mikopo katika Benki ya CRDB Tawi la Iringa mwaka 1997 na kutokana na utendaji wake mzuri, Juni mwaka 2000 alihamishiwa Makao Makuu na kuwa Meneja Uhusiano wa Mikopo ya Wateja Wakubwa.

Mwaka 2003 alipandishwa cheo na kuwa Meneja Mwandamizi wa Uhusiano wa Mikopo ya Wateja Wakubwa.

Baadaye benki ilimwezesha kwenda Uingereza kusoma Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara katika masuala ya benki na usimamizi wa fedha kimataifa katika Chuo Kikuu cha Birmingham.

Mwaka 2008 alijiunga na Benki ya NMB akiwa Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Wateja Binafsi na baadaye kuwa Mkuu wa Kitengo hicho mwaka 2013.

Mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati nafasi aliyodumu nayo hadi alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles