LIVERPOOL, ENGLAND
KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, Philippe Coutinho, amemtoa nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo, katika wachezaji watatu bora duniani kwa sasa.
Coutinho amekuwa akihusishwa kutaka kujiunga na klabu ya Real Madrid na Barcelona, lakini Liverpool wenyewe wamedai kuwa wanataka kumuongezea mkataba mpya ambao utamfanya awe ndani ya klabu hiyo kwa muda mrefu.
Coutinho amedai kuwa Ronaldo ana uwezo mkubwa wa kucheza soka, lakini kwa msimu huu kiwango chake hakiwezi kufanana na nyota watatu wa Barcelona, Lionel Messi, Luis Suarez pamoja na Neymar.
Hata hivyo, mchezaji huyo amedai kuwa katika kuwania tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2016, Ronaldo atakuwa na wakati mgumu wa kutwaa tuzo hiyo mbele ya nyota hao wa Barcelona.
“Nyota wangu watatu kwa ubora duniani ni MSN ambao ni Lionel Messi, Luis Suarez pamoja na Neymar, hao ni wachezaji hatari kwa sasa, wana uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo muda wowote, naweza kusema kwamba wachezaji hao wamekamilika,” alisema Coutinho.
Mchezaji huyo aliongeza kwa kusema kwamba, katika kuwania tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu, itakuwa ngumu kwa Ronaldo kwa kuwa mpinzani wake, Messi ameonesha kiwango kikubwa.
Coutinho kwa sasa atakuwa nje ya uwanja kutokana na kupata majeraha katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England mwishoni mwa wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Sunderland.
Kutokana na majeraha aliyoyapata mchezaji huyo, yatamfanya awe nje ya uwanja hadi mwakani wakati wa usajili wa Januari, lakini amewatoa wasiwasi mashabiki wa Liverpool mara baada ya kufanyiwa vipimo na kuanza kupata matibabu.