31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yapukutisha ajira

Na Avaline Kitomary

WAKATI watu zaidi ya 950,000 duniani wakielezwa kuambukizwa virusi vya corona, mamilioni wengine wamepoteza ajira ndani ya miezi mitatu.

Kwa upande wa Tanzania ingawa taarifa rasmi hazijatolewa na mamlaka husika, hoteli kadhaa zimefungwa huku sekta ya utalii ikielezwa kuzorota.

Zanzibar na mikoa ya kaskazini inatajwa kuathitika zaidi, huku wenye ajira za muda wakitajwa kuwa wahanga wa janga hili.

Wakati hali ikiwa hivyo nchini, Hispania wafanyakazi 898,822 wamepoteza ajira tangu Machi 12 ambazo zaidi ya nusu ni wafanyakazi wa muda.

Idadi ya watu ambao wameorodheshwa rasmi kuwa hawana ajira nchini humo, sasa wamefikia milioni 3.5 ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kutokea tangu Aprili 2017.

Marekani nako inaelezwa watu wasio na ajira wamefika milioni 6.65 ikiwa ni rekodi ya juu kuwahi kutokea kwenye taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani, sababu kubwa ikielezwa ni madhara ya corona na sasa asilimia 70 ya nchi watu hawaruhusiwi kutoka nje.

Hali hiyo inaelezwa kuwa mbaya zaidi kwa sababu watu wenye ajira za muda hawatanufaika na fao la kukosa ajira.

Wiki chache zilizopita, rekodi ilionyesha watu milioni 3.3 walikosa ajira, ikiwa viwanda vya magari vimesimamisha uzalishaji na sekta ya anga imeporomoka.

Nchini Uingereza nako Shirika la Ndege la British Airways linatarajia kupunguza wafanyakazi 36,000 kutokana na ndege nyingi kutofanya safari kwa sababu ya virusi hivyo.

Kwa wiki moja sasa shirika hilo limekuwa na mazungumzo na chama cha wafanyakazi kuhusu hatua yake hiyo.

Kwa maana hiyo, asilimia 80 ya wafanyakazi wa ndani ya ndege, mainjinia, wanaofanya kazi makao makuu na wale wanaohudumia ndege ikitua na wakati wa kuruka, watapoteza ajira.

MAT WATAKA DAWA ZA MUDA MREFU KUTOLEWA

Katika hatua nyingine, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimeomba Serikali kuweka sera ya matumizi ya muda mrefu ya dawa kwa baadhi ya magonjwa ili kupunguza mlundikano hospitalini.

Magonjwa yaliyotajwa kuweza kuwa na matumizi ya dawa hadi miezi mitatu ni kisukari, shinikizo la damu, maumivu ya mgongo na misuli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Rais wa chama hicho, Dk. Elisha Osati alisema kuwa utafiti mdogo walioufanya nchi nzima unaonyesha asilimia 70 ya wagonjwa wanaofika hospitalini ni wale wa marudio.

“Kwanza tunaipongeza Serikali na wadau wote ambao wanapambana na tatizo hili la corona. Lakini pia  tunaomba Serikali na wadau wengine kuwa bima ya afya  iruhusu kutoa dawa kwa wagonjwa wanaokuja kwa ajili ya marudio kwa miezi mitatu badala ya mwezi mmoja. 

“Kwa sababu pale wanapokuja kila mwezi kuongeza dawa, inaongeza hatari kutokana na wagonjwa kuwa wengi kliniki na uwezekano wa kuambukizwa unakuwa rahisi.

“Hao wenye matatizo mengine ndio wana uwezekano wa kupata ugonjwa mkali wakati mwingine kufariki, hata  yule mgonjwa aliyefariki kwetu tunaambiwa kuwa alikuwa na matatizo mengine, kwahiyo tunaomba hili ili kuweza kupunguza hivi visa,” alieleza Dk. Osati.

Licha ya kuwataka madaktari kuchukua tahadhari zaidi, pia aliiomba Serikali na wadau wengine kuhakikisha vifaa vya kujikinga vya kuwasaidia madaktari viweze kuwepo kwa uhakika.

“Tunawaomba madaktari wetu na watumishi wengine wa sekta ya afya wote waendelee kuchukua tahadhari  kwa sababu unaona mfano kama Italia madaktari kama 61 wana ugonjwa na karibu madaktari 20 wamefariki na  madaktari wanavyofariki sasa nguvu kazi inapungua, kwa hiyo ninawaomba waendelee kuchukua tahadhari. 

“Vifaa kama barakoa ambavyo tunatumia kujikinga mfano N95 ziwepo, lakini pia magauni ambayo tunavaa wakati tunahudumia wagonjwa wanaohisiwa au wale walithibitishwa kuwa na tatizo pia tunasisitiza madaktari wakiwa kazi muda wote wawe na mask, sanitizer na ndio maana tunaomba kuwa na uhakika wa vifaa hivyo,” alibainisha Dk. Osati.

Pia aliwaomba wananchi waendelee kuchukua tahadhari za kujikunga zinazoelekezwa na wataalamu wa afya ili kuweza kuepuka virusi vya corona.

 “Tunaomba wananchi waweze kutuelewa kwa sababu tunachojaribu kupambana nacho ni kitu ambacho bado hatujakijua vizuri.

“Kwahiyo tunavyowaambia kuwa mtu mmoja tu aje kumwona mgonjwa na pia tunavyowaambia wasije kliniki kama hawana tatizo wao waweze kuelewa kwa sababu maeneo ya hospitali yana hatari pia,” alisema Dk. Osati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles