30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

CoRI kukutana na wabunge mabadiliko sheria ya habari

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

TASNIA ya Habari nchini iko katika mchakato wa mabadiliko ya baadhi ya vifungu vinavyohusu Sheria ya Huduma za Habari nchini ambapo tayari muswada huo ulishawasilishwa bungeni tangu Machi 10, mwaka huu.

Hata hivyo, pamoja na kusomwa kwa muswada huo bado kumeonekana kuwapo na changamoto kwenye baadhi ya vifungu.

Neville Meena (aliyesimama) ambaye ni miongoni mwa wajumbe hao.

Hatua hiyo ndiyo imeisukuma timu ya Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), kwenda jijini Dodoma kwa lengo la kukutana na wabunge ili kufafanua zaidi mapendekezo ya mabadiliko ya vipengele vya sheria viliyoachwa nje kwenye muswada wa habari uliowasilishwa Februari 10, 2023.

Miongoni wa wajumbe hao wa CoRI ni pamoja na Deus Kibamba, Saumu Mwalimu, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Deus Kibamba, Mjumbe wa CoRI amesema, sababu kubwa ni kuhakikisha wabunge wanaelewa zaidi dhamira ya wanahabari na uhuru wa habari nchini.

“Bado tuna imani wabunge watatuelewa, tumekuja kukutana nao ili tueleze zaidi kwa nini baadhi ya vifungu vilivyoachwa nje ni muhimu kuingia kwenye muswada,” amesema Kibamba.

Upande wake, Wakili James Marenga, MISA TAN amesema wabunge ndio watunga sheria, na muswada umeishafikishwa kwao hivyo ni muhimu tukakutana nao.

“Tulianza na serikali na wakatusikiliza, wakawasilisha kile walichowasilisha bungeni. Ni wa kati sasa na sisi kukutana na wabunge kwa ufafanuzi zaidi, naamini wabunge ni waelewa na watatuelewa,” amesema Wakili Marenga.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema, kinachofanywa na CoRI (kukutana na wabunge) ni jambo la kawaida pale kunapokuwa na hatua za utungwaji wa sheria.

“Ni suala la kawaida pale panapokuwepo na hatua za utungwaji wa sheria, taasisi husika ikawa inatoa ufafanuzi zaidi juu ya kile inachopigania.

“Tumeona ni fursa kwetu sasa kukutana na wabunge ili kuwaeleza nini tunapigania na kwa nini. Nafasi hii tunapaswa kuitumia vizuri na ndio maana tupo hapa Dodoma,” amesema Meena.

Awali, akizungumza kwenye mkutano wa wadau hao uliofanyika jijini Dar es Salaam Februari 20, 2023 Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile alisema ni muhimu kwa CoRI kukutana na wabunge ili kushawishi baadhi ya vipengele ‘vilivyotelekezwa’ kwenye muswada huo.

“Tutakwenda kuzungumza na wabunge kuhusu athari zinazoweza kuifika tasnia ya habari kutokana na baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye sheria na marekebisho yaliyofanywa na serikali ili watusaidie kurekebisha siku wakianza kujadili bungeni,” alisema Balile.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile.

Balile alisema Bunge la sasa ni la bajeti lakini linaweza kubadili ratiba yake mwishoni na kuamua kupitia mapendekezo ya marekebisho ya sheria yaliyowasilishwa katika bunge lililopita.

“Tunafanya hivyo kwa kuwa huenda nafsi ikapatikana katika bunge hili, lakini ikishindikana basi itakuwa kwenye bunge la Septemba mwaka huu,” alisema Balile.

Miongoni mwa vipengele ambavyo CoRI wanapenda viingizwe kwenye muswada wa sheria kabla ya kujadiliwa ni pamoja na sehemu ya saba inayohusu adhabu na makosa yake ambapo walipendekeza kupungua adhabu hasa kwa makosa yanayohusu kitaalamu.

Walipendekeza serikali iondoe ukomo wa chini wa adhabu kwa vifungu vyote kwa kuwa inambana hakimu au jaji kuamua vinginevyo.

Na kwamba, sheria nyingi kwenye mataifa yaliyoendelea zinaweka ukomo wa juu wa adhabu kwa kuwa inatoa fursa kwa jaji au hakimu kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi husika.

Pia wanaeleza kifungu cha 7(2) kinaeleza kuwa serikali inaweza kutoa agizo habari fulani kuchapisha au kutangaza habari kwa kuwa ina umuhimu kwa Taifa.

CoRI wanaeleza, kifungu hicho ni kuingilia uhuru wa uhariri kwa kuwa, uhariri unafanywa nje ya chumba cha habari ambacho kina watu wenye weledi na uzoefu mkubwa.

CoRI wanalalamikia kifungu cha 5(e) a,b kinachohusu utoaji wa leseni ambapo Mkurugenzi wa Habari (Maelezo), anaweza kukataa maombi ya leseni au kuhuisha kulingana na matakwa yake.

Pia kinampa mamlaka ya kusitisha leseni wakati wowote anapoona chombo husika hakina mwenendo anaoutaka yeye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles