LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Klabu ya Chelsea, Antonio Conte, amesisitiza kuwa, bado wapo katika mapambano makali ya kuwania pointi 21 ili waweze kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini England msimu huu.
Baada ya kushinda mchezo wa juzi dhidi ya Stoke City kwa mabao 2-1, ilikuwa inaongoza Ligi ikiwa na pointi 13, lakini kocha huyo amedai kazi bado kubwa kuhakikisha timu yake inakuwa bingwa msimu huu.
Mchezo huo wa juzi ulionekana kuwa mgumu kwa Chelsea baada ya timu hizo kufungana 1-1, lakini Chelsea waliweza kipata bao lao la kuongoza katika dakika za lala salama na kumfanya Conte kuwa na furaha kubwa.
Kwa upande mwingine, klabu za Tottenham na Manchester City ambazo zinafukuzana katika nafasi za juu, zinahitaji kushinda michezo yote iliyobaki ili kuweza kumaliza ligi wakiwa na pointi 89, hivyo Conte amewataka wachezaji wake wajue kwamba, wapinzani wao wanaweza kushinda michezo yote iliyobaki.
“Bado tuna ushindani mkubwa wa kutwaa ubingwa, kwa sasa tunahitaji pointi 21 ili tuweze kuwa mabingwa msimu huu. Tumebakiwa na michezo 10 mbele na ushindani ni mkubwa, hivyo nimewataka wachezaji wangu kuendelea kupambana ili kushinda michezo iliyobaki,” alisema Conte.
Hata hivyo, kocha huyo amedai kuwa, wachezaji wake wamekuwa na furaha kutokana na maendeleo ya timu hiyo na wanaamini wanaweza kuchukua ubingwa msimu huu kama wataendelea kuwa na ushirikiano kama huo.
“Umoja wetu ndiyo chachu ya mafanikio yetu, uongozi pamoja na wachezaji tumekuwa kitu kimoja na ndiyo maana tunafanya vizuri kwenye michezo yetu,” aliongeza.