LONDON, ENGLAND
BAADA ya kupata pointi moja katika michezo mitatu ya Ligi Kuu England, kocha wa timu ya Chelsea, Antonio Conte, jana aliwapa onyo wachezaji wake kwa kuwataka warejee katika viwango vyao.
Kocha huyo aliwajia juu wachezaji wake hao baada ya kushuhudia juzi wakifungwa jumla ya mabao 3-0 wakiwa uwanja wa ugenini.
“Chelsea ni timu kubwa katika makaratasi tu, lakini si uwanjani, nataka iwe kubwa hata uwanjani kwani uwanja ndio sehemu sahihi kwa kuwa huko ndio sehemu inayofaa kuonesha uwezo.
“Kujituma na kupata matokeo mazuri ndio kitu muhimu ambacho ninichokitaka, hivyo tunatakiwa kufanya kazi ya ziada ili tufikie malengo,” alisema Conte.
Conte alisema msimu uliopita ulikuwa mbaya kwao na kuongeza kuwa hawatakiwi kufanya makosa waliofanya katika msimu huo, badala yake wanatakiwa kutafuta suluhisho sahihi ili kupata mwelekeo mzuri wa kupata ushindi msimu huu.
“Tunajua kuna vikwazo vingi katika kufikia lengo na hatujapata uwiano mzuri, ni muda sasa wa kusahihisha kila kitu kwani haikuwa sahihi kwetu kuruhusu kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Arsenal,” alisema Conte.
Mchezo dhidi ya Liverpool, Chelsea haikuwa katika kiwango kizuri kwani ilianza kuruhusu bao dakika ya 36 pia hali hiyo ilijitokeza hata katika mchezo wa Kombe la Ligi ya England (EFL), dhidi ya Leicester City walipoanza kufungwa dakika ya 34 kabla ya kupambana kupata ushindi dakika ya nyongeza.
Chelsea wamepata mabao 13 katika michezo nane ikiwa michezo saba bila ya beki wa timu hiyo, John Terry mwenye umri wa miaka 35.
Katika mchezo dhidi ya Arsenal, Conte alisita kumtupia lawama beki wake, Gary Cahill na kudai kuwa kila mmoja anatakiwa kuhusika na kipigo hicho.
Beki huyo anadaiwa kushindwa kufuata maelekezo ya kocha huyo hasa kipindi cha pili, ambapo alimtaka kucheza beki namba tatu.
“Tunatakiwa kutafuta suluhisho, kupoteza katika michezo miwili mikubwa, Liverpool na Arsenal.
“Kwa sababu hiyo, tunatakiwa kuelewa hali tuliyonayo, tunatakiwa kufanya kazi ili kuboresha kiwango chetu na kubadili historia,” alisema Conte.