NA SHOMARI BINDA,
KUANZISHWA Chuo Kikuu cha Kilimo na Sayansi cha Mwalimu Julius K.Nyerere wilayani Butiama kutaupandisha na kuuinua mkoa katika masuala mbalimbali na kuwasaidia wakulima kuinua kilimo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo,alipotembelea sehemu ya majengo ya iliyokuwa shule ya Osward Mang’ombe High School.
Majengo hayo ndiyo yatakayotumiwa na chuo hicho kinachotarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Oktoba mwaka mwakahuu.
Alisema chuo hicho ambacho kitatoa shahada na stashahada za fani mbalimbali licha ya masuala ya kilimo, kitakuwa chachu kubwa ya maendeleo ya Mkoa wa Mara na wananchi na kuwataka kujiandaa kukipokea.
Mulongo ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wa ngazi ya wilaya, alisema cha kwanza ambacho kinapaswa kuangaliwa ni kuhakikisha migogoro ya aina yoyote baina ya chuo na wananchi haizuki.
Hiyo ni pamoja na masuala ya ardhi ili uongozi wa chuo ufanye shughuli zake bila kubughudhiwa.
“Kwanza ni heshima kubwa kuwapo chuo hiki mkoani Mara na hususan kwenye Wilaya ya Butiama katika kumuenzi mzee wetu Mwalimu Nyerere na ni muhimu kinapokwenda kuanza kusiwapo na vikwazo vya aina yoyote,” alisema.
Alisema kutokana na taarifa ambazo amepewa na uongozi wa chuo hicho, wananchi wakulima wa kawaida pia watapata fursa ya kupata mafunzo ya muda mfupi ambayo yatawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na akawaomba wananchi kujiandaa na hilo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Profesa Lesakit Mellau, alisema hatua kubwa ya kuanza kwa chuo hicho imekwisha kufikiwa ikiwamo kuanza kuajili wahadhiri.