25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

CHUNUSI;  CHANZO NA JINSI YA KUZIEPUKA

Na JOACHIM MABULA


CHUNUSI ni tatizo la kawaida la ngozi linalowaathiri watu kipindi fulani cha maisha yao. Chunusi husababisha vipele vidogo vya mafuta kwenye ngozi na wakati mwingine hufanya ngozi kuwa na maumivu au kuhisi kuungua. Mara nyingi hutokea maeneo ya usoni, mgongoni na kifuani ambapo asilimia 15 ya wanaosumbuliwa na tatizo hili huwa na aina hii ya chunusi.

 

Kwanini unapata chunusi?

Mara nyingi chunusi huhusianishwa na mabadiliko ya kiwango cha homoni kipindi cha balehe. Hata hivyo, zinaweza kuanza katika umri wowote. Baadhi ya homoni zilizo jirani na vinyweleo vya ngozi hutengeneza kiwango kikubwa cha mafuta. Mabadiliko haya hufanya bakteria wanaoishi kwenye ngozi bila kusababisha madhara kukasirika na kusababisha vipele vyenye usaha.

Pia, homoni hufanya utando mnene chini ya vinyweleo vya ngozi na kusababisha kuziba kwa vijitundu vya ngozi hatimaye kusababisha chunusi. Kuosha ngozi hakusaidii kuondoa tatizo la vijitundu kuziba.

Unaweza pia kurithi tatizo la chunusi. Ikiwa baba na mama yako walikuwa na chunusi kipindi fulani cha maisha yao basi kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuwa na chunusi.

Mabadiliko ya homoni yanayotokea kipindi cha hedhi au ujauzito yanaweza kusababisha chunusi kwa wanawake. Hakuna uthibitisho kuwa lishe, uchafu au ngono huchangia kutokea/kutotokea kwa chunusi.

 

Kina nani huathirika zaidi?

Chunusi hutokea zaidi kwa vijana. Takribani asilimia 80 ya watu wenye chunusi wana umri kuanzia miaka 11 hadi 30. Chunusi hutokea zaidi kwa wasichana kuanzia miaka 14 hadi 17 na kwa wavulana ni kuanzia miaka 16 hadi 19.

Chunusi huja na kuondoka kwa watu wengi kwa miaka mingi ambapo miaka michache baadae hali hii huanza kupungua. Watu wengi hupona kabisa tatizo hili wakiwa na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea.

 

Nifanye nini nikiwa na chunusi?

Usioshe sehemu ya mwili yenye chunusi zaidi ya mara mbili. Kuosha mara kwa mara kunasababisha mikwaruzo na kufanya hali kuwa mbaya.

Osha sehemu ya mwili kwa sabuni kidogo ukitumia maji ya uvuguvugu na si maji ya moto au baridi kupita kiasi kwa sababu hufanya chunusi kuwa na hali mbaya zaidi.

Usijaribu kuviminya vipele au kuvisugua kwa nguvu kwa sababu hufanya ngozi kuuma na kutengeneza makovu ya kudumu. Jiepushe kutumia vipodozi na manukato kwenye ngozi yenye chunusi. Tumia bidhaa za urembo zisizoziba matundu madogo ya ngozi yako.

Ondoa vipodozi vyote ulivyopaka kabla ya kwenda kulala. Ikiwa una tatizo la kukauka ngozi ni vyema kuchagua mafuta/vipodozi vinavyopendekezwa na wataalamu wa ngozi.

Kufanya mazoezi hakuondoi chunusi ila husaidia kuboresha hisia za kujipenda zaidi. Ni vyema kuoga haraka iwezekanavyo baada ya kufanya mazoezi, kwa kuwa jasho husababisha ngozi kuwasha. Kama una nywele ndefu ziweke katika hali ya usafi mara kwa mara na epuka kuzifanya ziguse usoni.

Matibabu ya chunusi yanaweza kuchukua hadi miaka mitatu ili kuanza kuonyesha kupona, usitegemee kupata matokeo mazuri kwa usiku mmoja tu. Ingawa chunusi haziwezi kutibiwa, ila zinaweza kudhibitiwa kwa matibabu mbalimbali kama mafuta na losheni.

Ni vyema kuwasiliana na mtaalamu wa ngozi au mfamasia kabla ya kutumia dawa yoyote. Wakati mwingine kiuavijasumu(antibiotiki) huhitajika hasa chunusi zikizidi kifuani na mgongoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles